Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WA SEKTA YA AFYA WATAKIWA KUWATHAMINI WATUMISHI WA CHINI


Na. Catherine Sungura, WAMJW
Waganga wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (RRH) nchini wametakiwa kusimama katika nafasi zao na kuwatambua watumishi wa chini yao wanaofanya kazi kwa kujitoa kwenye kutoa huduma za afya pamoja na kusimamia upotevu wa mapato kwenye vituo vyao.


Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipofanya kikao na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora –Kitete.


Dkt. Gwajima alisema wapo watumishi ambao hawahitaji kuongozwa bali hujiongeza hivyo njia nzuri na yenye tija ni kuwatambua na kuwapa nafasi ya kuonesha vipaji vyao. Njia hii itaondoa malalamiko dhidi ya viongozi maana watumishi wote watakuwa wameshiriki kwenye kubuni mikakati yenye tija ya kuendeleza taasisi.


“Kila mtumishi asimame kwa nafasi yake ili kushawishi maendeleo ya eneo lake analofanyia kazi hususani katika vita hii ya uzalendo,lazima muwafurahie watumishi  wanaojitoa kwa kuwatambua  kwa mchango wao kwenye vituo vyenu kwa mazuri wanayoyafanya”.Alisema Dkt. Gwajima.


Dkt Gwajima aliwapongeza jumla ya watumishi watatu  na kuelekeza kuwa viandaliwe vyeti vya pongezi ili asaini kama kumbukumbu ya kutambua mchango wao kwenye maendeleo ya hospitali ya rufaa mkoa wa tabora, kitete. Watumishi hao ni Mohamud Ramadhani(MhasibuMsaidizi) na Nicholaus Okoth (Afisa Muuguzi Msaidizi)


Kwa upande wa mapato,waziri huyo aliwataka viongozi hao kuwa wazi kwa watumishi kwa kuonyesha mapato kwani watumishi wanakuwa gizani kwa kutokuona mapato na matumizi kwani fedha za hospitali ni fedha za umma na si za binafsi.


“Kila vitengo mnapaswa kukaa vikao kabla ya vikao vya idara na mtengeneze mfumo wa kusikiliza matatizo ya watumishi ili muweze kujua shida zinazowakabili watumishi wenu wa chini na muweze kuzitatua,tubadilike”.Alisisitiza Waziri Dkt. Gwajima.


Hata hivyo Dkt. Gwajima aliwataka maofisa ustawi wa jamii kufanya kazi na kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo kwa kuwa na mfumo wa kuwasaidia wenye matatizo  kwenye maeneo yao ya kazi kwani hivi sasa watu wengi wanateseka kwenye familia zao.


Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Mabula Mchembe amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kujituma kwenye nafasi zao kwani kila mmoja wanategemeana hivyo kufanya kazi kwa umoja itasaidia katika kurahisisha kazi kwenye hospitali yao.


Prof. Mchembe alisema njia moja wapo ya kuongeza mapato ni wao watumishi kuwa wabunifu na kuweza kuimarisha baadhi ya vitengo na wodi ikiwemo za kulipia ‘Private’ hiyo itachochea kuwa huduma bora na hivyo kuweza kuwanufaisha wao wenyewe.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com