Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIWANDA VYA NGUZO VYASHAURIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA


 Na Zuena Msuya Iringa,
Wamiliki wa Viwanda vya kuzalisha nguzo za miti za umeme washauriwa kujiandaa na kuanza kutumia teknolojia mpya ya kisasa inayokausha nguzo kwa kutumia mitambo maalumu badala ya mionzi ya Jua kama wanavyofanya sasa, ili kuongeza ubora na thamani ya nguzo hizo.

Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila alisema hayo, wakati wa ziara ya kutembelea viwanda hivyo na kutathmini njia zinazotumika kukausha nguzo pamoja na  kutoa ushauri kwa wenye  viwanda hivyo kujiandaa na kuanza kutumia teknolojia ya kisasa,badala ya mionzi ya jua kama inavyofanyika sasa.

Ziara hiyo ilifanyika Februari 04-05, 2021, katika Mikoa ya Iringa na Njombe, na ilihusisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Mhandisi Rwebangira alisema kuwa ziara hiyo pia ililenga kutoa ushauri kwa wamiliki wa viwanda hivyo ya namna bora ya kuboresha na kuimarisha viwanda vya ndani katika kuzalisha na kukausha nguzo bora na imara kulingana na soko la kimataifa Duniani.


Afafanua kuwa mwaka 2017, Serikali kupitia TANESCO, ilitoa maelekezo kwa viwanda vya nguzo kujianda ili kuanza kutumia teknolojia mpya ya ukaushaji nguzo kwa kutumia mitambo maalumu badala ya mionzi ya Jua, pia iliweka viwango vipya vya ubora wa nguzo za miti zitakazotumika katika miradi ya Umeme inayoendelea.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini kuwepo kwa mahitaji ya nguzo za aina hiyo katika miradi ya usambazaji umeme itakayoanza hivi karibuni na kwamba hakuna kiwanda chochote kinachotumia teknolojia hiyo hapa nchini.

“Kutokana na kukuwa kwa teknolojia, tunatarajia kuanza kutumia nguzo zakukaushwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika viwanda vyetu vya ndani, teknolojia hii huifanya nguzo kuwa imara na bora zaidi, pia hudumu kwa miaka mingi, hii itaondoa adha kwa wananchi ya kukosa umeme kwa sababu ya nguzo kuoza, kupasuka na kuanguka, hata hivyo teknolojia hii itakuza viwanda vyetu kwa kuuza nje nguzo zao”, alisema Mhandisi Rwebangila.

Aliendelea kuwasisitiza wenye viwanda vyote vinavyozalisha nguzo za miti za umeme nchini kuwa, ni wakati sahihi sasa kuweka mitambo hiyo katika viwanda vyao, ili nguzo hizo ziweze kununuliwa na kutumika katika miradi itakayoanzaa hivi karibuni.

Aliweka wazi kuwa, katika miradi hiyo mikubwa itayoanza hivi karibu, wakandarasi hawataruhusiwa kusambaza umeme kwa kutumia nguzo zilizoanikwa juani, nguzo zitazotumika ni zile tu zitakazokaushwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

“Wenye viwanda wekeni mitambo ya kisasa kukaushia nguzo, hatutanunua wala kuzikubali nguzo zilizokaushwa na miale ya jua katika miradi hii inayokuja, tutakuwa makini zaidi katika kuliangalia hili, tumewapa muda wa kutosha kamilisheni na waliobado wajenge, usipofanya hivyo ni kujiondoa mwenyewe sokoni”, alisisitiza Mhandisi Rwebangila.

Kwa upande wake Afisa Mthibiti ubora wa nguzo kutoka REA, Mhandisi Thomas Mbaga,aliwaeleza wenye viwanda hivyo kuwa REA haitakubali kupokea mradi wowote wa kusambaza umeme endapo nguzo zilizotumika si zile zinazotakiwa kwa viwango vilivyowekwa.

Vilevile alisema kuwa katika mikataba watakayotiliana saini na wakandarasi watakaopewa dhamana ya kutekeleza hiyo, itaeleza wazi nguzo zinazotakiwa hivyo mkandasi atayekaidi agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Naye msimamizi usambazaji wa umeme vijijni kutoka, TANESCO, Mhandisi Modest Mahururu alisema kuwa, shirika hilo limejiandaa kufanya ukaguzi wa kina kwa kila nguzo itayokuwa ikitumika katika miradi hiyo.

Aidha kwa kufanya hivyo kutaepusha athari na gharama za mara kwa mara zilokuwa zikisababisha na nguzo za umeme kuanguka kila wakati.

Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wenzake wa viwanda vya kuzalisha na kukausha nguzo za umeme, wa Kampuni ya Shedafa, Awadh Shedafa alieleza kufurahishwa kwao na ziara hiyo, kwakuwa ililenga kukuza uchumi wa viwanda vya ndani kwa kukuza soko la nguzo hadi nje ya nchi kulingana na ubora unaotakiwa, pamoja na kuongeza thamani na kuvilinda viwanda vyao.

Ameahidi kuwa kwa wale ambao wameanza kutekeleza agizo hilo wataongeza kazi zaidi ili kukamilisha kwa haraka uwekaji wa mitambo hiyo, na kwa waliobado waanza ili kutimiza lengo lililokusudiwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com