Ulimwengu unapoadhimisha sikukuu ya wapendanao, ama Valentine, kuna kundi la wanaume wanaojiita 'bahili' walioibuka katika mitandao ya kijamii ambao kwao sikukuu hii ni mwiko.
Kote barani Afrika, makundi mbali mbali yameanza mchakato wa kuandaa 'makongamano' ya wanaume, ama makundi ya wanaume bahili, katika kipindi hiki cha sikukuu ya Valentine.
Lakini lengo lao haswa ni nini?
Mwanahabari wetu Roncliffe Odit anaangazia chimbuko la makundi haya ya wanaume bahili, na kwa nini yana umaarufu mkubwa kote barani Afrika.
Kumekuwa na taarifa zilizotapakaa kuwa leo Jumapili Februari 14 ni siku ya pili ya Kongamano la Wanaume (Men's Conference).
Wajumbe kutoka mataifa mbali mbali waliwasili jana nchini Zambia, makao makuu ya Wanaume Bahali Afrika (Stingy Men Association of Africa).
Uwepo wao hapa nchini Zambia ni kwa ajili ya kuhudhuria 'kongamano' kubwa zaidi barani Afrika, Kongamano la Wanaume, ambalo linaandaliwa kwa mara ya pili sasa.
Si sadfa kwamba 'kongamano' hili linakuja wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Wapendanao (Valentine's Day) inayoadhimishwa Februari 14 kila mwaka. Muungano wa Wanaume Mabahili umekuwa ukiandaa 'kongamano' hili kwa mwaka wa pili sasa ili kuwaepusha wanaume na sikukuu ya wapendao.
Ukweli ni kwamba hakuna 'kongamano' la ukweli linaloandaliwa huko Zambia. Lakini kutajwa kwa 'kongamano' hilo kumetumika ili kuwatenga wanaume mabahili na sikukuu ya Valentine.
Lakini kwa nini wanaume kuwa mabahili?
Na mbona wanaume wanakataa kutumia hela zao wakati wa sikukuu ya wapendanao?
Mwangi Maina kutoka Kenya ni mwanahabari, na mshirika mkuu wa Kongamano la Wanaume.
Anasema wamelazimika kuja na 'kongamano' hilo ili kuzima mienendo ya kina dada kuwahadaa waume na kutumia hela zao wakati huu wa Valentine.
'Wanawake wengi ambao hawajaolewa hutumia sana sikukuu ya Valentines kufuja hela za wanaume. Ni lazima wakomeshwe,' anasema Maina.
Mwangi Maina pia ni muasisi wa mtandao wa Tutaoa Tukitaka (We Will Marry When We Want), ambao ni mtandao wa vijana wasio na haraka ya kufunga pingu za maisha. Na anasema sababu kubwa ya vijana wengi kutokuwa na haraka ya kuoa ni gharama kubwa inayohusishwa na mahusiano.
'Siku hizi mapenzi ni pesa, kama huna pesa hakuna msichana atakupenda. Kwa hiyo sisi tunatafuta pesa kwanza.'
Aidha maoni ya Mwangi Maina yanawakilisha asilimia kubwa ya wanaume kote barani Afrika ambao wameanza kujitenga na sikukuu ya wapendanao. Mitandaoni kumeibuka makundi mbali mbali ya wanaume bahili wanaojisifia kuwanyima hela wanawake.
Muungano wa Wanaume Bahili ulianzishwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Zambia baada ya mwanamume mmoja kwa jina Leonard Mweembe kukamatwa kwa madai ya kumpiga mkewe aliyemuomba hela za kusuka nywele mwezi Novemba 2020.
Kufikia mwishoni mwa mwaka jana, matawi kadhaa ya muungano huo wa mtandaoni yalikuwa yameibuka katika mataifa mbali mbali barani Afrika.
Muungano wa Wanaume Bahili Tanzania, Muungano wa Wanaume bahili wa Kenya, Wanaume bahili wa Uganda, na kadhalika
Baadhi ya kauli mbiu zao ni pamoja na 'acha nione ninachoweza kufanya' 'natarajia hela fulani wiki ijayo' ,' nina issue ninasikilizia' ambayo ni misemo ya udhuru wa kuwanyima hela wapenzi wao au wake zao.
Mwanamuziki wa Nigeria Don Jazzy pamoja na muigizaji wa Kenya Desagu ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao ni wanachama wa Muungano wa Wanaume Bahili Afrika.
Sikukuu ya Valentine huadhimishwa kila mwaka tarehe 14 Februari. Ni siku ambayo watu huonesha mapenzi kwa watu wao wa karibu kwa kuwatumia kadi, maua ama chokoleti zikiandamana na ujumbe wa mapenzi. Kitamaduni, wanaume ndio hutuma zawadi hizo kwa wanawake.
Wale wanaume mabahili wanaopinga maadhimisho haya wanahoji kwamba wanawake wamekuwa wakitumia siku hiyo kwa manufaa yao wenyewe. Baadhi ya wanaume hao wanadai kwamba mapenzi ni ya kila siku na hawafai kulazimishwa kutumia hela zao tarehe 14 Februari.
Lakini je, hilo lina ukweli wowote?
Soni Kanake ni mwandaaji wa kipindi The Garden of Eden nchini Kenya. Kwa mtazamo wake, wanaume wa siku hizi wanakwepa majukumu.
'Tangu siku za Mfalme Daudi, wanaume wamekuwa wakijitolea kutosheleza mahitaji ya wanawake wanaowapenda. Wengine hata wameua kwa sababu ya mapenzi, sasa watashindwaje kutumia mali zao kama kweli wanapenda?'
Soni, ambaye pia ni mwandishi wa vitabu kuhusu mapenzi na mahusiano, anahoji kwamba kizazi cha sasa cha wanaume mabahili wanatumia kisingizo cha hela kuwanyanyasa wanawake. Hata hivyo anasisitiza kwamba mwanaume akiwa amempenda kikweli mwanamke wake, basi hatahisi uchungu wowote kutumia hela zake.
'Unapata mwanamke mmoja analalamika jinsi mwaume wake ni mgumu wa hela, lakini mwaume huyo huyo anamwaga hela zake kwa mwanamke mwingine.'
Maoni yake yanaungwa mkono na Noel Mangoma, kijana barobaro kutoka Tanzania.
Noel anasema yeye haoni hasara kutumia pesa zake na mtu au watu wanaompa furaha ya kweli, kwani hakuna kiwango chochote cha pesa kinachoweza kununua furaha ya kweli.
'Mimi kwangu Valentine ni siku muhimu sana. Ni siku ya kusherehekea na mtu ninayempenda na kumthamini,' anasema Noel.
Yeye ni miongoni mwa wanaume wachache sana ambao wanapinga hoja ya kuwa na 'kongamano' kipindi hiki cha sikukuu ya Valentine.
Sikukuu ya Valentino inapotoshwa
Baba Padre Frederick Meela wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania anahimiza watu kuiheshimu na kuithamini hii siku takatifu
Father Meela anasema inasikitisha kwamba baadhi ya wanaume, na hata wanawake, wameipuuza ama kuidhalilidha siku hii kwa misingi ya pesa.
'Sikukuu hii asili yake ni Mtakatifu Valentino aliyeishi karne ya 3. Sikukuu yenyewe kiini chake ni upendo.Upendo usio na mipaka ya 'lazima unipe kitu' au masuala ya hela.'
Father Meela anashauri wanaume bahili waache kasumba hiyo, na wanawake ambao hutumia sikukuu ya wapendao 'kuchuna' wakome, bali watu wote wapendane.
Sasa wakati 'kongamano' la wanaume likiendelea hapa Zambia, na makundi ya wanaume mabahili yakiendelea kusajiliwa katika mataifa mbali mbali, swali linaloibuka ni, je, kuna mapenzi ya kweli bila hela?
Wakati ukisubiri jibu la swali hilo, wanaume wakarimu, wanaopenda bila kujali hela, wanaendelea kununua kadi, maua na chokoleti na kuwapelekea wapendwa wao matembezini katika maadhimisho ya sikukuu ya Valentine hii leo.
CHANZO - BBC SWAHILI