Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga hivi karibuni unaotekelezwa na halmashauri hiyo pamoja na Shirika la Rafiki SDO,Thubutu Africa Initiatives, Young Women Leadership, Shinyanga Press Club na halmashauri hiyo kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania (WFT). Kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba. Kulia ni Afisa Mradi wa Shirika la Women Fund Tanzania mkoa wa Shinyanga, Glory Mbia
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akizungumza Januari 22,2021 wakati akizindua Mradi wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga unaotekelezwa na Shirika la Rafiki SDO,Thubutu Africa Initiatives, Young Women Leadership, Shinyanga Press Club na halmashauri hiyo kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania (WFT). Wa kwanza kulia ni Afisa Mradi Shirika la Women Fund Tanzania mkoa wa Shinyanga, Glory Mbia akifuatiwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinaendelea kujitokeza katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kutokana na mila na desturi kandamizi, uoga wa kutoa taarifa pamoja na mfumo dume huku watu wa karibu wakiwemo ndugu wakitajwa kuwa ndiyo wahusika wa vitendo vya ukatili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Malunde 1 blog, baadhi ya wananchi katika kata Iselamagazi halmashauri ya Shinyanga wamesema uoga wa wanawake kutoa taarifa za vitendo vya ukatili vinachangia matukio hayo kuendelea kutokea.
“Wanawake wamejawa na hofu kuwa wakitoa taarifa za matukio ya ukatili wanayofanyiwa wataachika katika ndoa zao au kuonekana hawana nidhamu kwa waume zao kwa sababu jamii inaamini kuwa mwanaume siyo mtu wa kuulizwa kitu”,alisema Nyamizi Maganga.
“Tunashindwa kutoa taarifa za ukatili tunaofanyiwa na waume zetu kwa sababu ya uoga na hofu ya kuonekana tumeshindikana. Hizi mila na desturi zinatufanya wanawake tushindwe kuchukua maamuzi hata pale tunapoona watoto wanalazimishwa kuolewa au tunapopigwa majumbani”,alieleza Monica Nyanda.
Kwa upande wake, Leah Makoye alisema umefika wakati sasa jamii sasa iachane na mtazamo hasi wa kuwadharau wanawake kwa kila kitu kwani wanawake wana haki kama ilivyo kwa wanaume.
Naye Jacob Ramadhani aliwataka wanawake kubadilika kwa kupaza sauti dhidi ya vitendo wanavyofanyiwa kwani uoga wao wa kueleza yanayowasibu unasababisha vitendo vya ukatili viendelee kutokea katika jamii kwani hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wahusika.
“Hivi vitendo vya ukatili vinasababishwa na wanawake wenyewe. Mfano unakutana na mwanamke kavimba uso, ana majeraha yaliyotokana na kipigo lakini hawezi kusema ukweli kwamba kapigwa na mme wake matokeo yake anakwambia amejikwaa akaanguka au amegonga ukuta. Ni lazima wao kwanza wakubali kubadilika ili matukio ya ukatili yaishe”,aliongeza Ramadhani.
Joshua Madeleke aliwatupia lawama viongozi wa serikali za mitaa, kata na viongozi wa jeshi la jadi sungusungu kwa kuzigeuza kesi za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kuwa chanzo cha kujipatia mali na kumaliza kesi hizo kienyeji na kuwanyima haki waliofanyiwa ukatili.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba aliwataka wanawake kuvunja ukimya akisisitiza kuwa suala la ukatili siyo la kuvumilia.
“Wanawake wavunje ukimya, suala la ukatili wa kijinsia siyo la kuvumilika, watoe taarifa kwenye mamlaka zinazohusika na kwa bahati nzuri sasa namba zetu za simu zipo kwenye vituo vya afya,zahanati. Na wasipotoa taarifa maana yake wanakosa haki ya matatizo yao kushughulikiwa .Na sisi kama serikali kwa kushirikiana na wadau tunaendelea kutoa elimu jamii iachane na vitendo vya ukatili”,alisema Mahiba.
Mahiba alitaja moja ya mikakati kabambe ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kuwa ni kuzipa mamlaka serikali za vijiji kutunga sheria ndogo ambazo zitashughulikia suala la ukatili wa kijinsia katika maeneo ya ngazi ya vitongoji na vijiji.
“Nitoe rai kwa viongozi wa serikali za vijiji kwa kushirikiana na mamlaka zetu waweze kuwa na hizo sheria ndogo kwenye vijiji vyetu na hata linapotokea tukio la ukatili wa kijinsia iwe rahisi kushughulikia suala hilo kuanzia ngazi za vitongoji na vijiji kabla hata hawajafika ngazi ya halmashauri ili kupunguza mlolongo wa kushughulikia matukio ya ukatili kuanzia eneo la tukio hadi eneo la kupata haki hali inayosababisha wakati mwingine kupoteza ushahidi wa namna ya kumshughulikia mtuhumiwa”,alieleza Mahiba.
“Sisi halmashauri tumeshusha mamlaka haya ngazi za vijiji,serikali za vijiji zenyewe ziandae hizo sheria ndogo na hata likitokea tukio lolote mara moja ndani ya kijiji,chini ya kamati ambayo ipo ndani ya kijiji waweze kumshughulikia mtuhumiwa kabla hata ya kwenda kwenye vyombo vingine vya kisheria kama vile polisi na mahakama”,aliongeza Mahiba.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, hivi karibuni akizindua Mradi wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga unaotekelezwa na Shirika la Rafiki SDO,Thubutu Africa Initiatives, Young Women Leadership, Shinyanga Press Club na halmashauri hiyo kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania (WFT) alisema suala la Ukatili wa Kijinsia na watoto ni mtambuka ambapo kila mtu ana wajibu wa kushiriki katika kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii.
Kamanda Magiligimba alisema suala la ulinzi wa mtoto ni la kila mtu katika jamii na kusisitiza kuwa ni wajibu wa kila kiongozi kuanzia ngazi ya mkoa,halmashauri,kata na kijiji kuhakikisha wanakuwa na mipango mikakati ya kuzuia unyanyasaji wa mwanamke na mtoto katika himaya zao.
Alisema Sheria ndogo za kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia zitasaidia kila Mtendaji wa Kata au Kijiji kuhakikisha kwenye himaya yake hakuna mimba kwa wanafunzi wala ndoa za utotoni na kama zitatokea basi zifanyike juhudi kumpata mtuhumiwa ili kupata hukumu ambayo itakuwa fundisho kwa jamii ili iachane na vitendo vya ukatili.
Aidha alisema Jeshi la polisi kupitia kitengo chake cha Dawati la Jinsia na Watoto linapambana katika kukamata,kuhoji mashahidi pamoja na kuandaa majalada kwa ajili ya kwenda mahakamani akiongeza kuwa kazi ya kuendesha mashtaka mahakamani ni ya Idara nyingine hivyo wanafanya kazi kwa kushirikiana ili kuleta ufanisi katika mashauri.
Katika hatua nyingine alitoa wito kwa maafisa watendaji wa kata na vijiji waache kushiriki kumaliza kesi za ukatili wa kijinsia kifamilia.
Tayari Mkoa wa Shinyanga kupitia Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack umetengeneza Mpango Mkakati wa Mkoa katika kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ifikapo mwaka 2025 na umekuwa chachu ya mabadiliko katika mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Oktoba 12, 2020 Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, alisema Serikali ya mkoa huo ni ya kwanza hapa nchini kati ya mikoa 26 , kuzindua mpango wake mkakati wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Tumezindua mpango huu mkakati wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambao utadumu kwa muda wa miaka mitano, kuanzia (2020-2025) kwa kuonyesha dira ya mkoa, na kubainisha changamoto zilizopo katika mkoa wetu ambazo ni chanzo cha matukio haya na kuzifanyia kazi,”alisema Telack.
“Mashirika yote yasiyo ya kiserikali katika utekelezaji wao wa miradi ya mpango mkakati wa kitaifa wa Serikali wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA), watautumia mpango huu ambao tumeuzindua leo na kuwa kama dira yao,”alisema Telack.
Alisema kazi ya kuandaa mpango huo umefanywa na viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo mkoani humo, likiwemo Shirika la ICS, Women Fund Tanzania (WFT) ,Rafiki SDO, pamoja na AGAPE, ambapo pia walishiriki kufadhili uzalishaji wa nyaraka za vitabu na uzinduzi wa kitabu hicho cha mpango mkakati.
Aliitaka jamii ya mkoa wa Shinyanga,kuachana na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kuacha kuendekeza mila potofu ambazo ni kandamizi zilizopitwa na wakati akisema dhamira ya mkoa huo ni kuona kunakuwepo na usawa wa kijinsia kwenye nyanja zote, zikiwemo shughuli za kiuchumi, pamoja na watoto wa kike kuwa sawa kimasomo na wa kiume, na kuacha tabia ya kuwaozesha ndoa za utotoni na kuzima ndoto zao.
Social Plugin