Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza Muliro Jumanne akizungumza na waandishi wa habari leo
Na Hellen Mtereko - Mwanza
JESHI la polisi Mkoani Mwanza linawashikilia watuhumiwa 17 wa makosa mbalimbali ikiwemo mauaji ya familia, ubakaji, ukatili wa kijinsia, uporaji na utengenezaji wa pombe haramu aina ya gongo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 16, 2021 Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza Muliro Jumanne amesema, hatua hiyo inafuatia msako mkali uliofanywa na jeshi hilo kuanzia Januari mosi hadi Februari 16 mwaka huu na kufanikiwa kukamata gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T121 DHE.
Vifaa vingine vilivyokamatwa ni pamoja na pikipiki 6, Luninga 10, sabufa 4, simu za mkononi 51, mitambo 7 ya kutengenezea pombe aina ya gongo, pombe lita 100, Bangi KG 100, Mirungi KG 30 na kompyuta 2.
“Kufuatia msako huo mkali wa kata kwa kata, mtaa kwa mtaa nitahakikisha tunaunaongozwa na intelijensia ya jinai ili kuhakikisha hatukosei mtu lakini pia tunahakikisha tunapata sapoti ya wananchi kwenye ushahidi dhidi ya watu mbalimbali waliofanya makosa hayo,” alisema Muliro.
Kamanda Muliro aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bakari Hamiss (21) mkazi wa mtaa wa Mlimani B anayejihusisha na matukio ya mauaji, John Ezekiel (25) Amosi Lucas (19), Daniel Mussa (24) wakazi wa Kayenze watuhumiwa wa makosa ya ubakaji, Said Yusufu (24) Said Ramadhani (27) Hamisi Hussein (60) na Shaban Sarehe (9) wanaokabiliwa na makosa ya ubakaji.
Aidha Muliro alitoa tahadhari kwa wamiliki wa magari na madereva ambao magari yao yanadaiwa faini kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ambapo magari 510 yalikamatwa kutokana na makosa mbalimbali.
“Natoa wito, hizo faini ambazo zimetozwa kisheria baada ya wao kufanya makosa ni pesa ya serikali tusije tukalaumiana katika hili, magari yote ambayo yametozwa faini hii wao wenyewe wakalipe kabla ya msako mkali ambao umeshaanza”alisema Muliro