WAZIRI MKUU: WAZAZI TUWAPUNGUZIE WATOTO MAJUKUMU YA NYUMBANI
Tuesday, February 23, 2021
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wahakikishe wanawapunguzia watoto majukumu ya nyumbani na kuwawezesha kupata muda wa kujisomea na kupumzika.
Ameyasema hayo hayo leo (Jumanne, Februari 23, 2021) wakati akizungumza na walimu, wanafunzi na wazazi baada ya kukagua miundombinu ya shule ya Msingi Mitope, Ruangwa.
Waziri Mkuu amesema iwapo watoto watapata muda mzuri wa kujisomea na kupumzika itawasaidia katika kuwaongezea ufaulu kwenye masomo yao na kutimiza ndoto zao kielimu.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi wahakikishe wanafunzi wananunuliwa vifaa vyote vinavyohitajika shuleni kama sare, madaftari pamoja na kufuatilia mienendo yao kielimu.
”Wazazi tufuatilie na kujiridhisha kama watoto wetu wanafika shule na kuingia madarasani. Pia tuwe tunakagua madaftari yao na pale tunapoona hawafanyi vizuri tuwasiliane na walimu.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa amesema atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake kuendelea kusimamia vizuri shughuli za maendeleo.
Kadhalika, Mkuu huyo wa wilaya ameahidi kuendelea kusimamia vizuri fedha zote za maendeleo zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya wilaya ya Ruangwa ili zitumike ipasavyo.
Awali, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mitope, Margareth Mselewa alisema walimu wamejipanga vizuri kuhakikisha wanafunzi wote wa darasa la saba wanafaulu kwa asilimia 99.
Mwalimu huyo alisema katika matokeo ya mitihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka jana shule yao ilikuwa na jumla ya wanafunzi 21 ambao wote walifaulu na kwenda sekondari.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin