WAZIRI NDAKI ATAKA KUAINISHWA MIPAKA YA HIFADHI YA BAHARI KUONDOA MIGOGORO NA WAVUVI


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kata ya Kilindoni iliyopo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo na kutaka wavuvi waendelee na shughuli zao kwa kutumia taa kuvua samaki nyakati za usiku wakati wizara hiyo ikifanya tafiti zaidi za taa bora ambazo hazina madhara katika shughuli za uvuvi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akijadiliana jambo na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi) Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wakiwa kwenye boti maalum yenye kioo chini ambayo imewawezesha kujionea maeneo ya mazalia ya samaki yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, wakati Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili Wilayani Mafia. Pembeni ya Dkt. Tamatamah ni Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward Kondela

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekitaka Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kuhakikisha hadi kufikia Mwezi Agosti Mwaka 2021 kinaweka alama za mipaka katika maeneo yote ya hifadhi za bahari ili kuondoa migogoro kati yao na wavuvi.

Akizungumza jana (23.02.2021) na wananchi katika Kata ya Jibondo iliyopo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani, Waziri Ndaki ametaka kuwekwa kwa alama za mipaka hiyo baada ya baadhi ya wananchi kulalamikia kutozwa faini mara kwa mara kwa tuhuma za kufanya shughuli za uvuvi kwenye maeneo hayo ambayo hayaruhusiwi kisheria kwa shughuli hizo.

Aidha, Waziri Ndaki akiwa ameambatana na naibu waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul, amewataka wavuvi kuhakikisha pindi wanapokamatwa kwa makosa mbalimbali ambayo ni kinyume na sheria ya uvuvi kuhakikisha wanapatiwa risiti inayotambulika na serikali ya kieletroniki (EFD) na kuonya watumishi wa serikali wanaopokea fedha za faini bila kutoa risiti hizo.

“Tuweke mipaka ya hifadhi ieleweke hapa ndiyo mwanzo na hapa ndiyo mwisho, hadi mwezi wa nane maeneo tengefu yawe na mipaka yake ya hifadhi ya bahari, pia tushirikishe wananchi na viongozi wao siyo kuweka tu mipaka, pia kwa mtu anayekutwa na kosa la kwenda kinyume na sheria ya uvuvi akilipa faini apewe risiti ya serikali ya kieletroniki (EFD).” Amesema Waziri Ndaki

Pia, waziri huyo ametaka kufanyika kwa utafiti zaidi ndani ya mwezi mmoja juu ya matumizi ya aina mbalimbali za nyavu za uvuvi baada ya kupata malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wavuvi ambao wamekuwa wakilalamikia baadhi ya nyavu ambazo wanatakiwa kuzitumia kisheria kwa ajili ya uvuvi kutokuwa na sifa ya kukamata mazao ya samaki katika maeneo yao.

Amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah kuhakikisha kufikia Tarehe 23 mwezi Machi Mwaka 2021, awe amempatia taarifa hiyo ili iweze kutoa mwongozo wa maamuzi ya nyavu ambazo zina tija kwa shughuli za uvuvi.

Katika mkutano huo wa hadhara na wananchi wa Kata ya Jibondo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amepiga marufuku kitendo cha baadhi ya maafisa uvuvi kuwakamata wafanyabiashara wa samaki waliyopo mitaani yakiwemo maeneo ya kuuzia vyakula kwa madai samaki wanaouzwa katika eneo hilo hawana sifa kisheria badala yake watafute vyanzo vya maeneo ambayo watu wanavua samaki hao.

“Kuna mambo ambayo sipendi sitaki kabisa kusikia afisa uvuvi anaenda sokoni kutafuta samaki ambao wapo kinyume cha sheria na kuwanyanyasa akinamama wanaokaanga samaki, wakiona samaki wa namna hiyo wanapaswa kuwauliza aliyewauzia ili wapate chanzo halisi cha samaki walipovuliwa badala ya kumnyanyasa mfanyabiashara ambaye anauza chakula au kununua samaki anapeleka nyumbani kwa ajili ya mboga.” Amefafanua Waziri Ndaki

Kuhusu kilimo cha zao la mwani Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema zao hilo limekuwa likilalamikiwa kwa kuuzwa kwa bei ndogo hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima hao wasipate mafanikio na kuwataka wakulima wasiingie mikataba ya kuuza zao la mwani badala yake wauze kwa wafanyabiashara ambao wanakuwa na bei nzuri yenye tija kwao.

Dkt. Tamatamah amesema wizara itahakikisha inasimamia zao hilo kwa kuwa limekuwa mkombozi mkubwa kwa akinamama wengi katika Ukanda wa Pwani pamoja na kuwataka waliongezee thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Mhe. Juma Salum Ali amepongeza namna Wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyohakikisha inasimamia maeneo ya hifadhi ya bahari kupitia Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) huku akitaka kutatuliwa kwa baadhi ya changamoto ambazo zinaleta hali ya kitengo hicho kushindwa kushirikiana na wananchi.

Mhe. Ali amefafanua kuwa baadhi ya watumishi wa kitengo hicho wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa kufuata ueledi wa kazi yao na kuweka maslahi binafsi hali ambayo imekuwa ikizorotesha hali ya uhifadhi ukizingatia Wilaya ya Mafia bado ina maeneo mengi ambayo yana wingi wa samaki kwa ajili ya shughuli za uvuvi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliofika katika mkutano huo wamemuelezea Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo na kuelezea namna walivyo na imani kubwa na waziri huyo katika kutatua changamoto zao ili waweze kufanya shughuli za uvuvi bila bughudha na waweze kufuata sheria za nchi.

Aidha, Waziri Ndaki akiwa katika Kata ya Kilindoni Wilayani Mafia, amezungumza na baadhi ya wavuvi na kuwataka wafanye shughuli za uvuvi kwa kutumia taa nyakati za usiku wakati Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiendelea kufanya tafiti ya taa bora zaidi ambazo hazina madhara wakati wa kuvua samaki.

Mhe. Ndaki amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kulalamikiwa na baadhi ya wavuvi kushindwa kufanya shughuli zao nyakati za usiku kwa kuzuiwa kutumia taa kama chambo kwa ajili ya kukamatia samaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani akiambatana na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul ambapo Waziri Ndaki amepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wavuvi na kujionea hifadhi ya bahari na maeneo tengefu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post