Joyce Joliga Tunduru.
Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma imeunda kamati ya watu 9 kwa ajili ya kufuatilia na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria Wafanyabiasha wanaouza chumvi ambayo haina madini joto ili kunusuru watoto wenye umri chini ya miaka 5 wasipate udumavu wa akili.
Afisa Afya Wilaya ya Tunduru Ayub Joseph amesema kamati hiyo imeundwa kufuatia maagizo yaliyotolewa kwenye kikao cha Lishe kilichokaa mwishoni mwa mwaka 2020 baada ya kutolewa malalamiko ya wananchi kuuziwa chumvi ikiwa wazi kwenye magari makubwa ya mizigo huku ikipimwa kwenye vibakuri.
Amesema kikao kiliagiza Afisa Afya afuatilie wafanyabiashara hao ili kuweza kuwachukulia hatua ikiwemo kuwapiga faini na kuwafikisha Mahakamani ili kulinda afya za watoto wenye umri chini ya miaka 5 na udumavu wa akili pamoja na jamiii nzima na ugonjwa wa Goita.
Amesema wamekuwa walitoa elimu na maelekezo mara kwa mara kwa jamii na kufanya vipimo vya chumvi mashuleni, pamoja na madukani ili kupima madini joto ambapo baadhi imekuwa ikikutwa ina madini joto na nyingine imepungua madini joto kidogo kutokana na kutotunzwa vizuri.
"Tumeshawahi kumkamata mtu akiwa na chumvi mifuko 30 ya kilo 25 ambayo ilikuwa haina madini joto ambapo tulimwamuru aende kumwaga na tuliiteketeza yote", amesema
Amefafanua zaidi kuwa,sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009 inaeleza wazi kuwa iwapo utabainika unauza chakula chenye madhara kwa binadamu utalipa faini ya sh 500,000 au kuhukumiwa kifungo cha miezi 6 jela au vyote kwa pamoja. Na iwapo unajihusisha na kitu chenye madhara utapigwa faini ya sh 1,000,000 kwa au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
Kwa upande wake Mfanyabiashara Hornata Mwenda wa Tunduru aliwataka maafisa Afya kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiasha na ikiwezekana kushirikiana nao ili kuweza kukomesha tatizo hilo.
Naye Aziz Rashid Mkazi wa Mlingoti B Tunduru amewataka wananchi kuwa makini na chumvi wanazonunua ovyo mitaani kwenye matoroli ,au Malori yanayopitishwa mitaani kwao kwani nyingi hazina madini joto hali ambayo inasababisha madhara kwa Watoto na jamii .
Kwa upande wake Mganga Mkuu Wilaya ya Tunduru Dr.Wendy Robert ameahidi kushirikiana na Wataalam wa afya kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa kutumia chumvi yenye madini joto ili kujiepusha na madhara ya kiafya
Social Plugin