Mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli utawasili jijini Dodoma kesho jioni Jumapili Machi 21, 2021 na utalala Ikulu ya Chamwino na utaagwa katika uwanja wa Jamhuri Jumatatu Machi 22, 2021.
Akizungumza leo Jumamosi Machi 19, 2021 katika uwanja huo mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema mwili wa Magufuli utawasili katika uwanja wa ndege Dodoma saa 10:00 jioni na utapelekwa katika Ikulu ya Chamwino.
Amesema msafara wa gari litakalobeba mwili huo utapita barabara za Chako Chako, Nyerere, Bunge, Morena, Buigiri hadi Ikulu.
“Wananchi wote wa maeneo hayo mnaombwa kujipanga kwenye barabara hizo nilizozitaja ili kutoa heshima zetu za mwisho kwa mpendwa wetu,” amesema.
Amesema Jumatatu saa 12.00 asubuhi mwili utapelekwa katika uwanja huo kupitia barabara mpya ya Mfugale, Buigiri, Morena, Bunge, mzunguko wa mkuu wa Mkoa, Nyerere.
Amesema Jumatatu itakuwa siku ya mapumziko hivyo wananchi wataweza kujitokeza kwa wingi zaidi na shughuli hiyo itaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Via Mwananchi
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa
Social Plugin