Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika mji wa Kemondo mkoani Kagera.
Mradi wa maji wa Kemondo unatekelezwa kufuatia ahadi aliyoitoa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati akiomba kura mwezi Oktoba, mwaka 2020 kwa wananchi wa Kemondo.
Akizungumza na wananchi wa Kemondo katika mwendelezo wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameipongeza Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira kwa utekelezaji wa haraka wa miradi huo.
“Ni matumaini yangu kuona wananchi wa Kemondo wanapata huduma ya majisafi na salama mapema iwezekanavyo, hivyo tuna kila sababu ya kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huu kwa wakati”, alisisitiza Mhandisi Mahundi.
Alisema mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account) ukikamilika utahudumia kata sita zenye vijiji 17 kwa awamu 3 ambapo awamu ya kwanza itakuwa kata ya Kemondo yenye vijiji viwili hivyo litajengwa tenki la lita milioni 3, mtandao wa mabomba, (raising main) kwa gharama ya shilingi bilioni 6.8 na mpaka sasa wameshapokea shilingi milioni 600.
Awamu ya pili itagharimu shilingi bilioni 7 na itahusisha kata nne za Maruku, Kanyangereko, Bujugo na Katerero na awamu ya mwisho itahusisha Kata ya Muhutwe ambayo kazi zake zitagharimu shilingi bilioni 3.
Aidha, Naibu Waziri aliagiza ufanyike utaratibu wa kuongeza nguvu kazi ili vifaa vilivyopo katika eneo la mradi viweze kufanyiwa kazi kwa haraka na ikiwezekana kazi zifanyike usiku na mchana ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.
Pamoja na hayo, Mhandisi Mahundi alikagua mradi wa maji wa Kyaka Bunazi uliopo katika Wilaya ya Misenyi ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 48 na ukikamilika utahudumia wananchi wapatao 65,000 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.5, mradi huu unatekelezwa kufuatia agizo alilolitoa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Julai, 2019 ambapo aliagiza wananchi wa Bunazi wapate maji kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja.