Mwili wa Hayati Dk.John Magufuli ukiwasili katika uwanja wa Jamhuri Dodoma kwa zoezi la kuaga Kitaifa ambalo linaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,Marais 10 kutoka Mataifa mbalimbali,Viongozi pamoja na wananchi waliojitokeza.
Mjane wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli Mama Janeth Magufuli akilia kwa uchungu wakati wa zoezi la Kitaifa la kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Dk.Magufuli.
Baadhi ya Marais kutoka Mataifa mbalimbali waliofika katika kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli wakitia saini katika kitabu cha maombolezo kitaifa inafanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Sehemu ya wananchi waliofurika katika uwanja wa Jamhuri Dodoma kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kumuaga Hayati Dkt.John Magufuli kitaifa ukifanyika jijini Dodoma.
Wabunge mbalimbali wakitoa heshima za mwisho kwenye sanduku lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Hayati Dkt John Pombe Magufuli,kabla ya kupelekwa uwanja wa Jamhuri kwa kutolewa heshima za mwisho Kitaifa.
Mwandishi wa Habari wa Chombo cha EATV Bi OLiva Nyeliga akipiga saluti wakati akiaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli katika viwanja vya Bunge Leo Jijini Dodoma.
……………………………………………………………………………………………..
Na Alex Sonna,Dodoma
MAELEFU ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,Marais wa nchi zaidi ya 10 na viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania,viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na viongozi wastaafu wamefika Uwanja wa Jamhuri Dodoma kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk.John Magufuli.
Dkt.Magufuli ambaye amefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam ambako alikuwa anapatiwa matibabu kutokana na maradhi ya moyo katika mfumo wa umeme.
Wingi wa wananchi waliojumuika kwenye barabara za jiji la Dodoma wakiimba ‘Jeshi Jeshi Jeshi, Rais Rais Rais, Baba Baba Baba, Magu Magu Magu huku wengine wakilia ni uthibitisho tosha kuwa Dk Magufuli alikuwa kipenzi cha watanzania na wana-Dodoma.
Huzuni,Majonzi, vilio na simanzi vilianza kutawala bungeni kwa wabunge waliangua vilio na Simanzi wakati wakitoa heshima zao za mwisho za kumuaga Dk.Magufuli mara baada ya hapo mwili uliwasili katika uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo uwanja huo ulilipuka kwa Vilio na Simanzi kwa wananchi na viongozi waliofika.
Uwanjani hapo maelfu ya wananchi,viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania walianza kujitokeza mapema alfajiri ya leo Machi 22, 2021 ambao waliokuwa wametoka maeneo mbalimbali na wote wakiwa na hamu ya kushuhudia shughuli mbalimbali za kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk.Magufuli ambaye kwenye uongozi wake aliamini katika kuwasadia na kusikiliza wananchi wanyonge wenye changamoto mbalimbali za kimaisha.
Mwili wa Dk.Magufuli ulifikishwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma saa 10:43 asubuhi baada ya kutoka bungeni ambapo wabunge walitoa heshima zao za mwisho kumuaga Dk.Magufuli kabla ya wananchi na viongozi kutoka nchi mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho katika uwanja huo.
Pamoja na hayo kabla ya wananchi wakiongozwa na Rais Mhe.Samia pamoja na Marais 10 kutoka mataifa mbalimbali ambapo walikuja kutoa heshima zao za mwisho Kitaifa zilizofanyika hapa Dodoma Ibada maalum ilifanyika uwanjani hapo na wakati wa Ibada hiyo mengi yamezungumzwa kuhusu Dkt.Magufuli.
Ili kuwapa fursa wananchi katika kumuaga Chuma wa Afrika mwili huo utazunguka mara tano katika uwanja wa Jamhuri mara baada ya hapa utapitishwa katika mitaa maarufu iliyopo jijini Dodoma ambapo wananchi watajipanga kutoa heshima zao za mwisho.
Sehemu mwili wa Hayati Dk.Magufuli utapita na wananchi watatoa heshima zao za mwisho kwa kumuaga watajipanga katika Uwanja wa Jamhuri,Round about ya Bahi Road Via Shule ya msingi Uhuru,Iringa Road Via Mirembe Hospital,Barabara ya Kigamboni Via Kitto Bar na Central Police,Round about ya Jamatini,Barabara ya Bunge,Emmaus ya Pili mpaka Mataa,Barabara ya Mataa kuelekea kwa Waziri Mkuu/African Dream,African Dream kuelekea njia panda ya Wajenzi,Njia panda wajenzi kuelekea Airport.
Mara baada ya zoezi la kumuga Mpendwa wetu Hayati Dk.John Magufuli kumalizika jijini Dodoma kessho mwili utawasili visiwani Zanzibar Machi 23,Machi 24 itakuwa zamu ya Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani,Machi 25 mwili utaagwa Chato Mkoani Geita na Shughuli ya mazishi itafanyika Machi 26 wilayani Chato.
CHANZO - FULLSHANGWE BLOG
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa