Na Charles James, Michuzi Tv
NENDA SHUJAA! Ni maneno ambayo walikua wanayatamka wananchi wa Jiji la Dodoma waliojitokeza kwenye uwanja wa Jamhuri kumuaga aliyekua Rais Dk John Magufuli ambaye anaagwa leo kitaifa.
Mwili wa Dk Magufuli umeingia majira ya saa tano katika uwanja wa Jamhuri ambapo kila aliyekuwepo uwanjani hapa alisimama kumpa heshima kiongozi huyo mashuhuri aliyesifika kwa kusimamia nidhamu serikalini.
Wananchi waliojitokeza uwanjani hapa sambamba na viongozi mbalimbali wameshindwa kujizuia kumwaga machozi huku wengi wao wakiimba jina lake na kumtaka akapumzike kwa amani.
" Nenda shujaa nenda Baba, Nenda Jeshi! Hakuna tunalokudai umetupa Makao Makuu, umetupa hadhi ya Jiji umeibadilisha Dodoma hatuna tunachokudai, kazi kubwa uliyoifanya itaendelea kuonekana na kudumu kwenye maisha yetu," Ni baadhi ya maneno ya wananchi wa Jiji la Dodoma.
Mwili wa Dk Magufuli utaagwa na viongozi wakuu wa Nchi na Kimataifa leo jijini Dodoma ndani ya uwanja kisha utazungushwa mara tano kiwanjani hapa ili kuwapa fursa wananchi kumuaga na baadae utazungushwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dodoma ili kila Mwananchi aweze kutoa heshima zake
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa
Social Plugin