Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema baadhi ya wananchi walioshiriki shughuli ya kumuaga Rais John Magufuli wamejeruhiwa baada ya kukanyagwa na wenzao.
Mambosasa ameeleza hayo leo Jumapili Machi 21, 2021 alipoulizwa na Mwananchi Digital kuhusu taarifa za kuwepo kwa watu waliojeruhiwa na kukimbizwa hospitali katika shughuli hiyo iliyofanyika Uwanja wa Uhuru na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu.
Kutokana na wingi huo, shughuli ya kuaga ilisitishwa saa 9 alasiri na mwili wa kiongozi huyo ukiwa katika gari maalum ulizungushwa mara tano uwanjani hapo ili maelfu ya wananchi wapate fursa ya kuaga baada ya kuomba kutokana na kuelezwa kuwa wote hawataweza kupita mbele ya jeneza lililokuwa na mwili wa Magufuli.
Katika maelezo yake Mambosasa amesema idadi kamili ya watu waliojeruhiwa katika shughuli hiyo hana lakini ni wengi.
“Binafsi sina idadi lakini ni watu wengi ambao walikanyagana na kukosa hewa. Walikuwa wanaanguka na kubebwa,” amesema Mambosasa.
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa