Othman Masoud ateuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia tarehe 17 Februari mwaka huu.
Uteuzi wa Masoud umefanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi baada ya mashauriano na chama cha ACT-Wazalendo. Masoud amewahi kuhudumu katika nafasi za ngazi za juu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo mwanasheria Mkuu wa serikali.
''...Baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt Hussein Ali Mwinyi amemteua Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar'', imeeleza sehemu ya taarifa kutoka Ikulu ya Zanzibar kuhusu uteuzi huo.
Masoud anatarajiwa kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo kesho tarehe 2 Machi,2021.
Mteule huyo aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na alienguliwa katika wadhifa huo Oktoba 2014, na kisha akajiunga na upinzani awali chama cha CUF na sasa ACT Wazalendo.
Sura yake si maarufu katika siasa za upinzani lakini tangu afukuzwe ndani ya SMZ, amekuwa maarufu kwa misimamo yake ya kutetea maslahi ya Zanzibar katika Muungano.
Wakati wa pilikapilika za uchaguzi mkuu alikuwa mjumbe katika kamati ya ilani ya chama cha ACT Wazalendo kwa upande wa Zanzibar.
Licha ya madai ya kuibiwa kura na kuzuka kwa ghasia zilizopelekea vifo vya baadhi ya watu kufuatia uchaguzi wa mwezi Oktoba 2020, Chama cha ACT kiliingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif.
Hata baada ya kifo cha Maalim Seif baada ya kupata maambukizi ya virusi vya corona, chama hicho kinaendelea kuwa na haki ya kuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kuwa kilipata asilimia 19 ya kura za urais na kushika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita.
Masoud alikuwa ni miongoni mwa majina yaliyokuwa yanatajwa mitandaoni mwishoni mwa wiki hii baada ya chama cha ACT kutangaza kuwa walishapeleka jina kwa Rais Mwinyi kwa ajili ya uteuzi.