Katika tukio la kushangaza, mzee mwenye umri wa miaka 52 anadaiwa kumuoa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Bugire iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Vyanzo vyetu vya uhakika kutoka Rorya vimeeleza hivi karibuni kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 15 ameolewa na mwanaume huyo mwaka jana (2020) akiwa darasa la sita.
“Ina maana Januari mwaka huu (2021) huyu mwanafunzi huyo angekuwa darasa la saba,” kimeeleza chanzo chetu kutoka serikalini.
Taarifa zaidi zilizoifikia Mara Online News zinasema mwanaume huyo ametiwa mbaroni hivi karibuni na msichana huyo amerejeshwa kwa wanafamilia.
“Mzee aliyehusika kumuoa huyo mwanafunzi amekamatwa pamoja na mzazi wa msichana - aliyepokea ng’ombe wawili kama mahari wamekamatwa,” kimesema chanzo chetu.
Taarifa hizo zinadai kuwa mwanafunzi huyo ameolewa kuwa mke wa tatu wa mwanaume huyo.
“Kwa sasa anahitaji msaada hata wa kisaikolojia,” amesema ofisa wa serikali wilayani Rorya.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugire, Jackson Nyangubo amezungumza na Mara Online News na kuthibitisha tukio la kuolewa kwa mwanafunzi wake huyo.
“Ni kweli huyo msichana ni mwanfunzi wa shule yangu na watuhumiwa [muoaji na mzazi] tayari wametiwa mbaroni,” amesema Mwalimu Nyangubo.
Social Plugin