Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anaapishwa leo Ijumaa Machi 19, 2021 asubuhi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hafla ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan itafanyika Ikulu jijini Dar es salaam saa 4 asubuhi.
Kuapishwa kwa Mama Samia kunafuatia kifo cha Rais Dkt John Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 37 (5) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotungwa mwaka 1977, nafasi ya Urais inapokuwa wazi kwa sababu yoyote ikiwemo kifo, Viongozi watatu wameorodheshwa kushika wadhifa huo ambao ni Makamu wa Rais, na endapo hatakuwepo atachukua Spika wa Bunge na kama hayupo atachukua Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, baada ya kula kiapo cha Urais, atashauriana na chama chake cha siasa, ambacho kwa sasa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya wabunge wote.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais kufariki akiwa madarakani.