Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
**
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwaahidi Watanzania kwamba ahadi zote ambazo ziliahidiwa na aliyekuwa Rais Hayati Dk. John Magufuli yatatekelezwa ndani ya Chato na katika maeneo yote nchini.
Aidha ameihakikishia familia ya Hayati Dk.Magufuli kwamba Serikali itaendelea kuwa pamoja nayo wakati wote na msiba huo ni wa wote huku akiishukuru familia na Watanzania wote katika.kushiriki shughuli zote tangu alipotangaza kifo cha Dk.Magufuli.
Akizungumza leo Machi 26,2021,wakati wa ibada ya kumuombea Hayati Dk. Magufuli kabla ya kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Rais Samia amesema "Ndugu zangu mengi yamesemwa,lakini naungana na wote waliomshukuru Mungu kwa kufika siku hii ya kwenda kumsitiri mwenzetu,mpendwa wetu,kiongozi wetu.Nawashukuru viongozi wa dini wamekuwa na Serikali hatua kwa hatua.
"Nawashukuru wananchi wote, nawashukuru mataifa mengine kwa kuja kutufariji.Leo niko chato kwa mara ya tatu, mara ya kwanza wakati wa kampeni mwaka 2015, mara ya pili kaka yetu Rais Magufuli alipoondokewa na dada, na mara ya tatu ndio hii leo, tumekuja Chato kwa madhumuni ya kuja kumuweka kwenye nyumba yake ya milele.
"Nilipokuja wakati ule alionesha maeneo ambayo ndugu zake wamezikwa na sikudhani kama katika kipindi cha miaka nitakuja kwa ajili ya kumpumzisha yeye katika nyumba yake ya milele.Kwa familia naomba niwaambie msiba huu ni wetu sote hatutawaacha.Ahadi zote zitatekelezwa za hapa Chato na maeneo mengine",amesema.
Kuhusu ombi la Chato kuwa Mkoa, ambapo Rais Samia amewahakikishia wananchi wa Chato kwamba anazo taarifa mchakato umeanza,hivyo ameomba wapelekewe kuona kama vigezo vimekidhi na kama bado wataeleza nini kifanyike ili Chato ikidhi kuwa mkoa.
Kuhusu upungufu wa dawa,amesema amepokea na amelibeba ili kwenda kufanyia kazi."Kumekuwa na changamoto ya uhaba wa dawa lakini tumefanikiwa kuondoa changamoto hiyo,na kama kuna upungufu wa dawa maana yake kuna tatizo katikati, tutafanyia kazi."
Wakati huo huo,Rais Samia amesema anaishukuru kamati ya mazishi kwa kufanya kazi kubwa huku akisisitiza kuishukuru familia pamoja na ofisi binafsi ya Dk.Magufuli."Familia imetoa kila aina ya ushirikiano, tumekuwa wamoja.Naomba niungane na Spika , kimetokea cha kutokea lakini Mungu hatuacha,atatushika mkono, mpendwa wetu tuombee.
"Dk.Magufuli ameitwa na Mungu ameitika,leo hapa tunapumzisha kiwiwili chake tu lakini maono na mitazamo yake kupitia kauli mbiu ya Hapa Kazi tu itaendelea,ninachowaomba Watanzania twendeni tukiwa tukashimane, tuijenge Tanzania yetu.