Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)kwa kushirikiana na wadau wake katika ngazi ya jamii na ngazi ya taifa, wanaratibu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka mnamo tarehe 08 Machi. Maadhimisho haya ni ya kipekee katika harakati za Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi, kwani kwa namna ya kipekee wanawake na wadau wanaotetea haki za wanawake huja pamoja kusherekea mafanikio waliyofikia, kutafakari changamoto zinazoendelea kuwakabili na kupanga mikakati ya jinsi ya kuzitatua kwa kutumia fursa zilizomo katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, vikundi na kitaifa (kimfumo).
Kwa mwaka huu, kauli mbiu ya
kidunia ya siku ya wanawake duniani inasema “Wanawake
katika Uongozi: Fanikisha Usawa katika Dunia yenye COVID-19”. Kitaifa, Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa
na kauli mbiu isemayo: “Wanawake Katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa”.
Kwa namna ya kipekee, tumejipanga
kufanya maadhimisho haya ya siku ya wanawake duniani kwa kipindi cha mwezi huu
mzima wa tatu tukiongozwa na mada kuu ya kidunia na kitaifa, ambapo ujumbe wetu
mkubwa ni “Badili
Mitazamo kuleta Usawa”na
kwa vile lengo kuu ni kuangazia wanawake katika uongozi, tunaongozwa na msemo
wa #ViongoziTuwaandaeSasaKwa ujumla, maadhimisho haya ya
Siku ya Wanawake Duniani yanalenga:
· Kutambua na kusherekea mafanikio ya
wanawake katika kupambana na mifumo isiyo Rafikikatika sekta mbalimbali
· Kuweka mikakati yenye lengo la
kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za uongozi wa aina mbali
mbali-kisiasa, sekta binafsi, ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na Tanzania yenye
usawa wa kijinsia
· Kujadili kwa kina umuhimu wa kuthamini
mchango wa mwanamke ndani ya jami na zaidi kuangazia ongezeko la kazi zisizo na
malipo na kuweka mikakati ya kupunguza mzigo huo wa kazi kwa wanawake
· Kuongeza mijadala katika Jamii juu
ya simulizi na kauli zisizojenga na zisizo na tija kwa ustawi wa wanawake na
maendeleo ya Jamii na ufanya ushawishi kwa jamii ili kuongeza ushiriki wao
katika kujenga simulizi chanya na zenye tija kwa wanawake na Jamii kwa ujumla
·
Kuhakikisha
kuwa maeneo muhimu yanayozalisha maarifa na ujuzi,yanaweka mazingira muhimu ya
kumjenga ewezo na kujiamini mtoto wakike kama sehemu ya maandalizi ya kuwa
kiongozi wa baadae. #ViongoziTuwaandaeSasa
Jumla ya matukio makubwa matano
yatafanyika katika mwezi huu mzima wa Machi kama sehemu ya kuadhimisha siku ya
Wanawake duniani. Matukio hayo ni:
· Ziara
ya kwenye vyombo vya habari katika ngazi ya kitaifa na kijamii kuanzia tarehe
5-30 Machi 2021. Ziara hizi zinalenga kuendelea kutoa elimu kwa Jamii na kuibua
mijadala itakayopelekea Jamii kuchukua hatua kuelekea mabadiliko chanya
· Uzinduzi
rasmi wa mikakati yetu kuelekea siku ya Wanawake Duniani kwa vyombo vya habari
tarehe 6 Machi 2021.
· Maadhimisho
katika ngazi ya jamii “Dunia tuitakayo kwa wanawake na watoto wa kike” (The
Future We Want for Women and girls)– Tarehe 7-20 Machi 2021
ü TGNP
kwa kushirikiana na Vituo
vya Taarifa na Maarifa katika
Halmashauri 18 katika mikoa 9 nchini tutafanya maadhimisho haya katika
ngazi ya jamii ili kutambua na kusherekea wanawake walioleta mabadiliko na
maendeleo katika maeneo yao.
ü Kupitia maadhimisho haya tutaweza
kuandika na kuweka kumbukumbu ya wanawake mashujaa katika ngazi ya jamii kutoka
kwenye halmashauri hizo, ambao wataibuliwa na wanajamii wenyewe.
ü Wanavituo vya Taarifa na Maarifa pia
wataunganishwa na vyombo vya habari ngazi ya jamii ili kuweza kuujulisha umma juu
ya ajenda yao ya kuwatambua na kuwasherekea wanawake hao ili kuleta chachu kwa
wanajamii ndani na nje ya maeneo yao; kutambua na kuthamini mchango wa wanawake
katika maendeleo na hivyo, kubadili mitazamo yao juu ya uongozi wa wanawake,
hivyo, kuweza kuongezaushahidi ni kwa nini umma, wake kwa waume wanapaswa
kuhakikisha wanawake wanaongezeka katika nafasi za uongozi ili kuongeza chachu
ya mabadiliko na maendeleo katika taifa letu na dunia kwa ujumla.
·
Kilinge
cha Simulizi – tarehe 10 Machi 2021
ü TGNP
imekuwa ikiratibu Kiilinge vya simulizi tangu mwaka 2017 ambapo kimekuwani
jukwaa mahususi linalowaleta pamoja vijana, wanafunzi na wanaharakati/ viongozi
waliobobea katika Nyanja mbalimbali wakimwemo wanawake walio katika sekta
zilizo na wananume wengi zaidi,ili kubadilisha uzoefu na kujifunza kutokana na
simulizi za safari zao hadi kufikia walipofika.
ü Kilinge hiki kitatumika kama sehemu
ya kuwalea watoto wa kike kujiandaa kuwa viongozi na kuhamasika kuingia katika
tasnia za sayansi na technolojia ambazo zinaaminika kuwa ni za wanaume.
·
Kampeni
ya Kubadili namna ambavyo jamii imekuwa ikieleza kuhusu mwanamke (Changing
Naratives) tarehe 11 Machi 2021.
ü Kama
sehemu ya muendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, TGNP kwa
kushirikiana na WFT na TAMWA,tunaandaa mjadala utakaofanyika mtandaoni mwenye
lengo la kubadili simulizi hasi katikajamii ambazo zinadhalilisha, kuwanyong’onyesha
na kuondoa utu wa mtu, thamani yake na ujasiri wake.
ü Mjadala
huo unategemea kuleta pamoja washiriki mbalimbali wakiwemo vituo vya taarifa na
maarifa, wasanii wa kike na wa kiume, wakilishi kutoka vyombo vya habari,
wahamasishaji wa mitandao ya kijamii, wawakilishi kutoka TCRA, vinara wa jinsia
wanaume wakiwemo wabunge.
· Kongamano la pili Wanawake na
Uongozi (Women and Leadership Summit) tarehe 16-17 Machi 2021
ü Kongamano
la kwanza lilizinduliwa rasmi na TGNP mwaka 2018 kwa lengo la kuhamasisha
ushiriki wa wanawake katika uongozi na nafasi za kufanya maamuzi katika nyanja
mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
ü Kongamano
la Wanawake na Uongozi ni jukwaa linaloleta kwa pamoja wanawake viongozi mahiri
na wanawake viongozi chipukizi au wanaotia nia ya kuwa viongozi wakiwemo vijana
wa kike ili kuweza kubadilishana mawazo na kujifunza kwa lengo la kuongeza wigo
wa ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.
ü Kongamano
hili la Pili linatarajiwa kuwaleta pamoja viongozi mbalimbali katika siasa,
uchumi kwa lengo la kushirikisha uzoefu, kuwezeshana na kuweka mikakati ya
kuongeza idadi ya wanwake viongozi katika majukwaa hayo.
· Ziara ya Vijana katika vyuo vikuu kuanzia
tarehe 20-24 Machi 2021:
ü Kwa
kushirikiana na Jukwaa la Vijana wa kike wanaharakati (YFF), tunatarajia kuwa
na ziara katika vyuo vikuu vya nne vilivyopo Dar es salaam (Chuo kikuu cha Dar
es salaam, Mzumbe, Mwalimu Nyerere na IFM) ili kutambua na kusherekea uongozi
wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi wa wanafunzi hasa kwa wale
wanawake walioweza kushika nafasi za urai au makamu wa rais katika serikali ya
wanafunzi kwenye vyuo hivyo.
ü Pia,
katika ziara hizi, tutaweza pia tambua michango ya vijana walioweza kuhamasisha
mabadiliko katika jamii.
ü Kubwa
zaidi ni kuendelea kuvuta vijana kujiunga na kukwaa hili wakiwa vyuoni lakini
pia, kuanzisha majukwaa kama haya wakiwa katika maeneo wanayoishi ili kuleta
mabadiliko katika jamii wanazotoka. Katika maadhimisho haya vijana hawa
watakuwa na ujumbe mbalimbali watakaofikisha kwa jamii pia kwa njia ya mitandao
ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.
ü Kupitia
ziara hizi pia, vijana hawa wataweza kuhamasisha uundwaji wa vitovu ya jinsia
vyuoni vyenye lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo Jinsia na
maendeleo.
Tunapozungumzia
ushiriki wa wanawake katika uongozi tuangalie katika mapana yake. Jinsia ni
suala la Maendeleo hivyo hatuna budi kwa pamoja kutoa kipaumbele ili kuongeza
ushiriki wa wanawake wenye tija katika Maendeleo. Ni kwa mantiki hii TGNP
tumeamua kuandaa matukio hayo niliyoeleza hapo juu kama sehemu ya kutoa fursa
kwa wanawake na wadau wengine kutafakari wapi tumefanikiwa, wapi bado kuna
changamoto na kupanga mikakati ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika ngazi
zote za maamuzi pamoja na uongozi.
TAKWIMU:
Takwimu za IPU (2019) zinaonesha kuwa hadi Januari 2019, wanawake wakuu wa nchi (Head of state) walikuwa 10 kati ya 152 (asilimia 6.6) tu ambapo wanawake wakuu wa Serikali (head of government) walikuwa 10 kati ya 193 (asilimia 5.2). Kwa upande wa Afrika kwa sasa kumekuwa na marais wanne wanawake, aliyekuwa rais wa Malawi, Joyce Hilda Banda (Aprili 2012- Mei 2014), aliyekuwa rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf (Januari 2006-Januari 2018), aliyekuwa raisi wa Mauritius Ameenah Gurib-Fakim (June 2015- March 2018) na Rais kutoka Ethiopia Sahle-Work Zewde (Octoba 2018 hadi leo).
Vile
vile, takwimu zinaonesha kuwa hadi January 2019, kidunia maspika wabunge wanawake
ni asilimia 19.7 na manaibu speaker wanawake ni asilimia 28.2. kulingana na
ripoti hiyo hiyo, Wabunge wanawake katika nchi zote walikuwa ni asilimia 24.3.
ambalo ni ongezeko la asilimia 13 kutoka asilimia 11.3 mwaka 1995. Pia kufikia
2020 kulikuwa na wastani wa wabunge wanawake 24.4%. katika nchi zilizo kusini
mwa Jangwa la Sahara ambalo ni ongezeko la asilimia 14.6 tangu mwaka 1995.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofanya vizuri katika ushiriki wa wanawake katika uongozi. Kulingana na takwimu za Interparliamentary Union (IPU) hadi 2020, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki na nafasi ya 23 duniani kwa kuwa na 36.9% ya wanawake wabunge ambapo Rwanda imeshika nafasi ya kwanza hadi kidunia kwa kuwa na 61.3%. Hata hivyo, bado hatujaweza kufikia 50/50 na hivyo, hatuna budi kuongeza juhudi katika kuongeza nafasi za wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi ili kufikia malengo.
Kwa Tanzania, kwa mara ya kwanza
baaada ya uhuru tumeweza kuwa na mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa raisi Mhe.
Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameweza kushika nafasi hiyo kwa awamu mbili
mfululizo toka 2015-2020 na awamu hii ya 2020-2025. Hii ni hatua ya kupongezwa
katika nchi yetu. Vile vile kwa mara ya
kwanza katika nchi yetu bunge la 10 tumeweza kupata spika wa Bunge mwanamke
Mhe. Mama Anne Makinda na katika bunge la 11 na la 12 tunaye naibu Spika wa
bunge Mhe. Dr Tulia Akson. Hata hivyo katika kamati za Bunge uwakilishi wa
wanawake kama wenyeviti wa kamati ni
mdogo sana. Kwa upande wa wabunge wa
kuchaguliwa, wanawake ni 25 ya wabunge 264 wa kuchaguliwa ambayo ni sawa na
asilimia 9.5% tu ya wabunge wote; idadi ya wabunge wanawake wa viti maalumu ni
113 ambayo ni sawa na asilimia 29 ya wabunge wote. Jumla ya wabunge wanawake ni 142 sawa na
asilimia 37 ya idadi ya wabunge wote ambao ni 393. Hii bado ni idadi ndogo ukilinganisha na
lengo la kufikia asilimia 50/50.
Uwakilishi wa wanawake katika nafasi
za uongozi wa kisiasa katka ngazi ya udiwani bado ni changamoto kubwa. Licha ya
juhudi za wadau mbalimbali ambazo zinafanyika ikiwemo seriali asasi za kirai na
wadau wa Maendeleo. Takwimu zinaonesha kuwa (NEC, TEMCO) kwamba idadi ya
madiwani wanawake wa kuchaguiwa kutoka kwenye kata ni 204 ambayo ni sawa ana
asilimia 5 ya madiwani wote. Madiwani wanawake wa viti maalumu ni 1,611 Sawa na
asilimia 30 ya madiwani wote. Kwa ujumla wanawake madiwani ni 1,815 sawa na
asilimia 33.9 ya madiwani wote. Madiwani
wa kuchaguliwa ndio wenye fursa za kugombea na kushika nafasi ya mwenyekiti wa
halmshauri ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa mkutano mkuu wa baraza la madiwani la
Halmashauri ambalo lina mamlaka ya kujadili na kupitisha bajeti ya
halmashauri. Kwa bahati mbaya ushiriki
mdogo wa wanawake madiwani wa kuchaguliwa unawanyima wanawake wengi kushika
nafasi za uenyekiti wa halmashauri. Tanzania bara ina jumla ya halmashauri 185
ambapo ni Halmashauri 6 tu sawa na asilimia 3.2 ambazo zinaongozwa na wawanake
wenyeviti.
Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 80
ya wananchi wanaishi katika ngzi ya vijini na kata na chimbuko la maendeleo ya
nchi ni katika ngazi hiyo. Hivyo, ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi hizo
muhimu na za kimkakati ni changamoto katika kuleta usawa wa kijinsia na
maendeleo jumuishi na endelevu.
Ikumbukwe
kuwa serikali yetu imeridhia mikataba na matamko mengi ya kuleta Usawa wa
Jinsia na Maendeleo katika ngazi za
kimataifa na kikanda.; yakiwemo:Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR:1948),
Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW:
1979), Mpango Kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo, na Mkataba wa
Hiari wa Jinsia na Maendeleo kusini mwa Africa (SADC Gender and Development
Protocol,) mikataba hii inaelekeza serikali husika kuhakikisha wanawake
wanapewa nafasi sawa na wanaume katika ngazi mbalimbali za uongozi. Vile vile
Tanzania Dira ya Maendeleo ya 2025 (TDV 2025) imetambua kuwa mojawapo ya
vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na jamii yenye muono wa kimaendeleo
ambapo pamoja na mambo mengine unakuwa na tamaduni wezeshi hususani kwa
wanawake na makundi mengine.
Licha ya juhudi hizo za kuridhia matamko na mikataba bado wanawake wanakutana na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha Maendeleo yao hasa ushiriki wao katika nafasi za maamuzi. Tofauti za utajiri na za kijinsia zinaongezeka, katika nchi zinazoendelea zikiwa na ufinyu wa utajiri, maarifa na teknolojia. Wanawake maskini wa mijini na vijijini wanazidi kusukumwa pembezoni, wakionekana kama siyo sehemu ya jamii. Tafiti zinaonesha kwamba nchi za Afrika zinapoteza takribani dola za kimarekani 105 milioni kwa mwaka kwa kutowaingiza wanawake katika uchumi. Pia takwimu zinaonesha kuwa wanawake ni zaidi ya asilimia 70 ya wakulima wadogo ambao ndio wanalisha nchi yetu. Wanawake walioko katika sekta isiyo rasmi ni asilimi 51.1% ambapo wanaume ni 48.9%. Vile vile ni 20% tu ya wanawake wanamiliki ardhi. Ufikiaji wa huduma za jamii bado ni changamoto hususan kwa wanawake kwani licha ya jitihada za kumtua mama ndoo Kichwani bado vijijini wanawake wanatumia muda mwingi kati ya masaa 3 hadi 5 kutafuta maji. Huduma za afya, hasa afya ya uzazi ni changamoto kwani bado wanawake wanakufa kwa wingi kwa vifo vya uzazi kati ya vizazi 100,000 tunapoteza wanawake 556, kwa upande wa elimu pamoja na kupongeza jitihada za elimu bure bado watoto wetu wa kike wanashindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa vifaa na mazingira ya kujihifadhi wakati wakiwa katika siku zao za mwezi.
Kwa
mawasiliano zaidi:Wasiliana nasi kupitia idara ya mawasiliano na habari
1. Monica
John
Simu:
0652 267 611
Barua
Pepe: monica.john@tgnp.or.tz
2. Jackson
Malangalila
Simu:
0657 479 490
Barua
Pepe: jackson.malangalila@tgnp.or.tz
3. Asteria
Katunzi
Simu:
0711 407 222
Barua
Pepe: Asteria.katunzi@tgnp.or.tz
Social Plugin