KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE UCSAF YATOA MSAADA KWA YATIMA


Baadhi ya watumishi wa Mfuko wa Mawasiliano  kwa wote [UCSAF] wakiongozwa na Mtendaji Mkuu katika zoezi la kukabidhi vifaa kwa uongozi wa kituo. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi Justina Mashiba na kushoto ni Sr. Aurea Kyara mlezi wa watoto kituoni hapo.
Baadhi ya watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Nyumba ya Matumaini wakimsikiliza Sr. Aurea Kyara[ hayupo pichani] wakati wa kupokea vifaa vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote [ UCSAF].
Watumishi ( wanawake wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote[ UCSAF] wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa kituo cha Nyumba ya Matumaini pamoja na walezi wao mara baada ya kupokea vifaa hivyo
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Bi. Justina Mashiba [kulia] akizunguza na waandishi wa Habari mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa kituo.

 Na: Celina Mwakabwale 

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ( UCSAF) umetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Nyumba ya Matumaini kilichoko kata ya Miyuji, Halmashauri ya jiji la Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wanawake wa Mfuko waliofika kituoni hapo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Bi. Justina Mashiba ametoa wito kwa wanawake hasa viongozi kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa uadilifu na ufanisi mkubwa huku wakiendelea kutambua kuwa wao ni wazazi na walezi wa familia hivyo wasisahau majukumu yao ya kifamilia.

Aidha ameongeza kuwa, baadhi ya familia zimekuwa kwenye migogoro ambayo imepelekea unyanyasaji na kutengana kwa wazazi hali ambayo inachangia ongezeko la watoto yatima pamoja na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Bi Mashiba ameongeza kuwa, ili taifa liendelee kuwa na watoto waliolelewa katika misingi bora ya kifamilia, wanawake hasa viongozi wanatakiwa kutambua kuwa nafasi za uongozi walizonazo si mbadala wa majukumu yao katika familia.

"Napenda kuwakumbusha wanawake wenzangu, kuwa unapokuwa katika majukumu ya kikazi yatekeleze kwa ufanisi lakini unaporudi nyumbani kwako wewe ni mwanamke, wewe ni mama, tusilisahau hilo"

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo kwa niaba ya kituo, Sr. Aurea Kyara ameishukuru taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote huku akitoa wito kwa taasisi na wadau wengine kuendelea kujitolea katika kusaidia kituo hicho pamoja na vituo vingine kama hivyo.

Akielezea baadhi ya changamoto wanazokutana nazo, Sr. Kyara amesema, baadhi ya ndugu wa watoto hao huwatelekeza baada ya kupeleka kituoni hapo baada  ya wazazi kufariki dunia.

Kutokana na hilo, baadhi ya watoto wamekuwa wakikataa kurudi kwenye familia zao muda unapofika, hali ambayo inasababisha kituo kuendelea kuwa na idadi kuwa ya watoto.

"Tunawaomba ndugu wa watoto, wanapowaleta hapa wasiache kuja kuwatembelea, watoto wanatakaa kurudi nyumbani kwa sababu hawaifahamu familia hivyo inakuwa ngumu kwao kuishi na watu ambao ni ndugu lakini hawajawahi kuwaona", aliongeza Sr. Kyara.

UCSAF imetoa msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo mchele, maharage, sabuni za kufulia na kuogea, unga wa ngano, mafuta ya kupikia pamoja na taulo za kike vyenye thamani ya shilingi milioni 4 na nusu za kitanzania.

Siku ya kimataifa ya wanawake huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi maadhimisho yaliyoanzishwa kwa lengo la kupinga mazingira duni ya kazi na vitendo vya unyanyasaji katika ajira.

Nchini Tanzania maadhimisho ya siku hiyo kwa mwaka 2021 yatafanyika kimkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.  Ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni  "Wanawake katika uongozi: chachu kufikia dunia yenye usawa.

Imetolewa na kitengo cha uhusiano/ Mawasiliano [ UCSAF]

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post