Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI TARIME WATAKA TAKWIMU ZA WENYE MAAMBUKIZI YA VVU ZIWEKWE WAZI

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wakijadili taarifa ya robo ya pili ya 2020/2021.

Na Dinna Maningo,Tarime

Madiwani wameitaka halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kuweka wazi takwimu za watu waliopima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwenye makablasha ya taarifa zijazojadiliwa kwenye vikao ya Baraza la Madiwani.

Walisema kuwa takwimu za Ukimwi zinapowekwa wazi zinasaidia kufahamu ni maeneo gani yenye maambukizi makubwa na maeneo ambayo hayana maambukizi mengi ili kuwawezesha wadau mbalimbali kuzidi kutoa elimu ya UKimwi na wananchi kujikinga zaidi. 

Madiwani waliyasema hayo wakati Mwenyekiti wa kamati ya Ukimwi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri Victoria Mapesa wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Ukimwi (CMAC) ya robo ya pili 2020/2021 kwenye kikao cha baraza la Madiwani ambapo ilikosolewa kwa kutokuwa na takwimu za Ukimwi.

Akisoma taarifa hiyo Mapesa alisema kuwa shughuli zilizofanyika ni pamoja na madhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambapo huduma za upimaji VVU, tohara kwa wanaume, uchunguzi wa saratani ya kizazi, uchangiaji damu na huduma za macho zilizotolewa. 

Akizungumzia suala la utoaji wa Kondomu alisema kuwa ugawaji wa Kondomu kupitia shirika la PSI lilitoa kondomu zipatazo 37,152.

"Taarifa ya Ukimwi kutoka Idara ya Afya inahusu huduma ya upimaji wa VVU kwa kila vituo, hali ya upimaji kati ya wanaume na wanawake, huduma ya upimaji VVU kwa watoto chini ya miaka 14,hali ya magonjwa ya ngono (zinaa) huduma ya upimaji kwa wajawazito na huduma za wateja wanaotumia dawa za ARVs",alisema. 

Baada ya taarifa hiyo Diwani wa kata ya Kwihancha Ragita Mato aliikosoa taarifa hiyo kwa kutoonyesha takwimu za upimaji wa VVU kwa wanaume, wanawake, wajawazito, watoto takwimu za magonjwa ya Ngono na wagonjwa wanautumia dawa za ARVs. 

"Ni vizuri tujue takwimu za hali ya maambukizi ya VVU magonjwa ya ngono kwanini hamjaziandika? ni lazima tujue kama maambukizi ni mengi au yameshuka, tujue waliopima VVU walikuwa wangapi kati ya hao waliokutwa na maambukizi ni wangapi ambao hawana ni wangapi, hivyo hivyo kwa wajawazito, watoto, wanaume kwa wanawake na tujue wangapi wamejiunga kutumia dawa na ambao hawatumii dawa za ARVs.

"Hali ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa hatujui wangapi wamepimwa walikuwa na magonjwa yapi, je ni kaswende au kisonono lakini taarifa haionyeshi,zaidi tu ya kutuambia tu upimaji usiokuwa na takwimu sasa tutajadili nini kama hakuna takwimu ambazo ndiyo zingetuwezesha kujadili kujua hali ya maambukizi ikoje ili tutafute ufumbuzi wa tatizo"alisema Mato. 

Diwani wa kata ya Gwitiryo Nashon Mchuma alisema "Tulishakaa vikao tulifuatilia tukaambiwa kuwa hatupaswi kuonyesha takwimu kwamba zinabaki kuwa siri, sisi hatuhitaji majina yao sisi tunataka kujua takwimu yaani takwimu zinakuwaje siri!?.

 "Madiwani tutaelewaje hali ya kuenea kwa virusi vya Ukimwi unampaje mtu elimu ya VVU bila kuwa na takwimu zake ambazo zitakupa dira uanzie wapi uishie wapi, unatoa elimu kwa wananchi kwamba tujihadhari na Ukimwi ni hatari unaua wanakuuliza ni hatari kwa kiasi gani au umepungua kwa kiasi gani utawajibu nini?"alisema. 


Diwani wa viti maalumu Mariam Mkono alisema kuwa takwimu za Ukimwi ni lazima zitolewe ili Madiwani wafahamu kwa kuwa ndiyo wenye wananchi huku akisisitiza elimu ya Ukimwi iendelee kutolewa kwa kuwa kwa sasa kumekuwa kimya na watu wakidhani Ukimwi haupo hali ambayo inaweza kusababisha kuongezeka kwa maambukizi ya VVU. 

Mkono aliongeza kuwa ni vyema viongozi wa dini wakazidi kutoa elimu kwa wananchi kuachana na uzinzi, wakielezwa kuwa uzinzi ni dhambi itasaidia baadhi kuacha na kumrejea Mungu.

Kaimu Mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Tarime Joseph Ngowi alisema kuwa takwimu za maambukizi zipo kwenye zahanati, Vituo vya afya na hospitali ya halmashauri na kwamba maeneo yanayoongoza kwa maambukizi makubwa ya Virusi vya Ukimwi ni Nyamongo, Sirari na Nyamwaga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com