Na Ripota wa Michuzi Blog, Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaambia Wabunge na Watanzania kwamba mengi yamezungumzwa kuhusu aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk.John Pombe Magufuli lakini kwake imekuwa siku ngumu kwani kila anapoangalia jeneza anahisi kama vile anapigiwa simu anapewa maagizo na maelekezo.
Majaliwa amesema hayo leo Machi 22,2021 katika Viwanja vya Bunge Mjini Dodoma kabla ya Wabunge kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk.Magufuli na kumuombea Dua ambapo amesema "Sina kubwa la kusema, waliotagulia wamesema mengi kuhusu mpendwa wetu.Binafsi napata shida kusema, naona kama vile ananipigia simu, ananipa maagizo, naomba mnivumilie, ni siku ngumu kwetu.
"Kila mmoja ana neno la kumuelezea Dk.Joh Magufuli, tukianza kuelezea hatutamaliza, amefanya mambo mengi kwenye majimbo yetu, tunachokifanya leo hapa ni kumuombea dua, ni majonzi makubwa kwetu, na sio kwetu tu Watanzania bali Afrika inamlilia, inasikitika, nchi za SADC ,Bara la Afrika linamlilia, alikuwa sehemu ya viongozi wa bara hili, hivyo majonzi haya siyo ya kwetu peke yetu.
"Jukumu letu ni kumuombea, tunamlaza katika nyumba yake ya milele machi 26, leo tumepata fursa ya kuja kumuombea, kwa uzoefu ambao tumeupata Dar es Salaam watu walikuwa wengi sana, hivyo kwa hapa Dodoma tumeamua kubadilisha utaratibu, badala ya kwenda kuaga na kumuangalia, tutakachofanya ni kuzungusha mwili mara mbili au tatu uwanjani,"amesema.
Ameongeza kuwa baada ya hapo mwili wa mpendwa wetu Dk.Magufuli utapitishwa katika barabara."Hivyo leo tuko hapa, kesho Zanzibar, halafu mwanza na kisha Chato ambako nao watapata nafasi ya kumuaga kwa siku nzima,"amesema Waziri Mkuu.
Aidha amesema wakati wakimuombea Dk.Magufuli na kumuaga katika viwanja hivyo vya Bunge, mama mzazi wa Dk.Magufuli yupo kitandani kwa mwaka wa pili amelala, hivyo Watanzania tumuombee mpendwa wetu na wakati huo huo tumuombee mama yetu apate nguvu na aweze kunyanyuka kitandani.
Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zeberi Ally Maulid wakati anazungumza mbele ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge, Waziri Mkuu na viongozi wengine waliokuwepo viwanja vya Bunge, Maulid amesema katika kipindi cha miaka mitano na miezi mitatu ya Rais Magufuli kuna mabadiliko makubwa katika taifa letu, amefanya mambo makubwa ambayo yanaonekana kwa macho.
"Kila anapopita umati unaokusanyika kwa ajli ya kusherehekea yale ambayo yamefanyika ni mkubwa sana sana, lakini hata enzi za uhai wake alipokuwa anapita watu walijitokeza kwa wingi na alikuwa anasimama na kutoa neno la matumaini.Pamoja na uongozi wake mzuri, bado amekuwa mwalimu kwa viongozi tulio wengi.
"Na ndipo tunapopata matumaini kwetu tuliobakia tutaendeleza yale ambayo ameyeaacha na kufanya ubunifu wa kufanya mengine kwa ajili ya Taifa letu.Rais Magufuli aliwahi kusema enzi za uhai wake nchi yetu ni tajiri na yeye hakuwa sehemu ya wanaotaka kujilimbikizia mali, alikuwa mtu mwenye upendo kwa Watanzania wote.
"Kilichobakia kwetu ni kuendelea kumuombea, Rais Magufuli ni nuru na nyota iliyozimika ghafla. Tumuombee dua kwa Mwenyezi Mungu, tunajua alikuwa binadamu hivyo huenda wako aliowakosea, hivyo wamsemehe."
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa
Social Plugin