Charles James, Michuzi TV
TUMEMPOTEZA Rafiki! Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imempoteza mwanamageuzi wa kweli na rafiki ambaye aliziunganisha Nchi zote zinazounda Jumuiya hiyo.
Akizungumza katika uwanja wa Jamhuri zinapofanyika shughuli za kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk John Magufuli, Rais Kenyatta ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na watanzania kwa ujumla kufuatia kifo cha Dk Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.
Rais Kenyatta amesema kwenye uongozi wa Dk Magufuli aliwafundisha wana-jumuiya ya Afrika Mashariki kujitegemea kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuacha kutegemea misaada kutoka mataifa ya Nje.
"Afrika imempoteza mwanamageuzi wa kweli, mimi binafsi nimempoteza rafiki wa kweli ambaye tulipigana simu kila siku tukishirikiana katika mambo mbalimbali ya kujenga mataifa yetu.
Kwako Dada yangu Rais Samia Suluhu Hassan barabara umeoneshwa, sisi tupo nyuma yako nikuombe uendeleze kazi kubwa iliyoanzishwa na ndugu yetu Dk John Magufuli, niwaombe watanzania muungane mumpe ushirikiano Rais Samia ili aweze kuendeleza falsafa ya Dk Magufuli ya Hapa Kazi Tu, " amesema Rais Kenyatta.
Amesifu jitihada kubwa zilizofanywa na Dk Magufuli katika kipindi chake cha uongozi kwa kujenga miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, ujenzi wa kisasa huku akisema mchango wake katika ukuaji wa uchumi hautofutika kwa miaka yote.
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa
Social Plugin