HISTORIA FUPI YA MAISHA YA RAIS MAGUFULI


Kwa kawaida, katika jamii yoyote ya wanadamu, kuzaliwa kwa mtoto ni suala la shangwe. Hicho ndicho kilichotokea Alhamisi ya Oktoba 29, 1959 katika Kitongoji cha Katoma, Kata ya Bugando, Tarafa ya Nzela, Wilaya ya Geita, alipozaliwa John Joseph Magufuli.

Miongoni mwa walioshuhudia kuzaliwa kwake, hakuna hata mmoja alijua kwamba miaka 56 baadaye mtoto huyo angekuja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi duniani.

Dr Magufuli alipata elimu ya msingi kati ya mwaka 1967 na 1974 katika shule ya msingi Chato, na kisha kujiunga na Seminari ya Katoke kwa elimu ya sekondari kati ya mwaka 1975 na 1977.

Baadae aliendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Lake jijini Mwanza na kumaliza kidato cha nne mwaka 1978.

Mwaka 1979 alijiunga na shule ya sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa ambapo alihitimu mwaka 1981, na mwaka huohuo akajiunga na chuo cha ualimu Mkwawa ambapo alihitimu Stashahada ya elimu katika Sayansi akijikita katika masomo ya Kemia na Hisabati.

Rais Magufuli alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambapo alihitimu shahada ya kwanza ya sayansi katika kemia na hisabati mwaka 1988.

Mwaka 1994 alihitimu shahada ya Uzamili katika sayansi, na hatimaye kuhitimisha safari ya elimu kwa kupata shahada ya uzamivu mwaka 2009 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Maisha ya siasa

Safari ya kisiasa ya Rais, Dkt. John Magufuli ilianza kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi ambayo sasa inaitwa Chato mwaka 1995, na mwaka huo huo aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Mzee Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Nyota ya Rais Magufuli ilizidi kung’ara katika ulingo wa siasa ambapo mwaka 2000 alichaguliwa tena kuwa Mbunge wa Chato, na kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyoishika hadi mwaka 2005.

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Rais wa wakati huo Jakaya Kikwete alimteua Dkt. Magufuli kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mwaka 2010, alirejeshwa tena katika Wizara ya Ujenzi na kufanya kazi kubwa ya kujenga barabara kadhaa nchini kote kwa kipindi kingine cha miaka mitano hadi mwaka 2015 ambapo aliamua kujitosa kuwania urais wa Tanzania.

Kazi ilikuwa kubwa ambapo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Magufuli aliwashinda wagombea wengine zaidi ya 40, na baadaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Tano wa Tanzania.

Rais Magufuli alishinda pia nafasi hiyo kwa kipindi cha pili katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 mwaka 2020.

Kipindi cha pili cha Urais wa Dkt Magufuli kilianza kwa kiapo cha Novemba 5 mwaka 2020, ikimaanisha kuwa amekaa madarakani kwa siku 132 pekee.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post