KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA UJENZI WA JNHPP
السبت, مارس 13, 2021
Na Zuena Msuya Pwani,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula amesema Kamati hiyo imeridhishwa na kasi ya Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere( JNHPP) na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mradi huo.
Kitandula alisema hayo tarehe 12 Machi, 2021 mkoani Pwani, wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo inayolenga kukagua maendeleo ya Miradi mbalimbali katika sekta ya Nishati inayotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
Alisema kuwa baada ya kuona hali halisi ya utekelezaji wa mradi huo kwa sasa Kamati hiyo inatembea kifua mbele ikijivunia kazi kubwa iliyofanyika na inayoendelea kufanyika kukamilisha mradi huo kwa wakati.
“Kwa mara ya kwanza wakati wazo la kutekelezwa kwa mradi huu lilivyotolewa, Kamati tulifurahia sana kuona ndoto ya Baba wa Taifa inaenda kutimia na kuweka historia mpya ya nchi yetu, na tuliadidi kuwaeleza watanzania mpaka watuelewe juu ya mradi huo mkubwa unaogharimu fedha nyingi, kwakuwa sisi ndiyo wenye dhamana ya kupitisha bajeti ya Serikali pamoja na miradi yake, baada ya kuona kinachoendelea hapa sasa hivi, tunatembea kifua mbele na kuwaeleza watanzania kuwa wajivunie kuwa na mradi huu mkubwa utaokamilika ndani ya muda uliopangwa na utakuwa na manufaa makubwa sana ndani na nje ya nchi”, alisema Kitandula.
Aidha alisema kuwa, wamefurahishwa na kitendo cha Serikali kulipa kwa wakati fedha za mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa kila hatua ya ujenzi wa mradi inapofikia.
Sambamba na hilo aliipongeza Serikali ya awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. John Magufuli kwa kuthubutu na kutekeleza mradi huo, ulioasisiwa na Baba wa Taifa zaidi ya miaka 40 iliyopita, na kuupa kipaumbele kwa kutenga fedha za kutekeleza mradi husika.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani aliieleza Kamati hiyo kuwa imekuwa ni chachu ya kutekeleza mradi huo baada ya kuridhia na kupitisha bajeti ya kutekeleza mradi huo pamoja na kuwa bega kwa bega na wizara ya Nishati kuhakikisha mradi huo unatekelezwa.
Dkt.Kalemani alisema kuwa mradi JNHPP utakaozalisha megawati 2115 umetoa fursa kwa wahandisi wataalam kupata elimu na ujuzi zaidi wa kujenga mradi mwingine kama huo.
Aliweka wazi kuwa takribani Wahandisi wa ndani 200 wamepata Mafunzo ya namna ya kujenga miradi kama hiyo katika vyanzo mbalimbali vya Maji yanayopatikana nchini.
Vilevile aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa tayari ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme kutoka katika mradi huo hadi katika kituo kikubwa cha kupokea na kupoza umeme kilichopo Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma kupitia Dar es Salaam- Chalinze Pwani umeshaanza kutekelezwa.
“Ninyi Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ndiyo mmefanikisha utekelezaji wa mradi wa JNHPP kwa kuridhia na kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati ambayo ndani yake kulikuwa na fedha nyingi za kutekeleza mradi huu ambazo ni fedha za ndani, bila kuchoka mmekuwa mkifuatilia matumizi ya fedha zinazotumika katika mradi huu ukilinganisha na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi, tunaamini ushirikiano baina yenu na sisi ndiyo umeleta matokeo chanya kwa watanzania na Taifa kwa jumla”, alisisitiza Dkt.Kalemani.
Katika hatua nyingine aliwaomba wajumbe wa Kamati hiyo kwa kushirikiana na Kamati nyingine, kuwa mabalozi wa kuhamasisha ulinzi wa vyanzo vya Maji ya mito inayotiririsha Maji yake katika mradi wa JNHPP.
Dkt.Kalemani alisema kuwa, kuanzia mwenzi Novemba mwaka huu, kingo za maji ya bwawa zitakuwa zimekamilika na kuanza kuvuna maji Maji yatakayotumika kuendesha mitambo ya kufua Umeme pindi mradi huo utakapokamilika Juni 2022, hivyo ni muhimu kutunza vyanzo vya mito na kuwa na matumizi sahihi ya Maji ya mito.
Alisema kuwa, zaidi ya futi za ujazo Lita Bilioni 32. 5 za maji kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mito zinahitajika ili kuanza kujaza maji katika bwawa hilo hivyo taasisi, mashirika mbalimbali pamoja na watu wanaoishi kuzunguka vyanzo maji ya mradi huo wanatakiwa kuwa walinzi wakuu, kulinda maji yasipotee bila sababu ya msingi.
Aliongeza kuwa, Mradi huo utakapokamilika mwaka 2022 utazalisha Megawati 2115, na kuifanya Tanzania kuwa na Jumla ya Megawati 4848, huku mahitaji halisi kwa nchi zima yakitarajiwa kuwa ni Megawati 2700.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza gharama ya Umeme na kuongeza usambazaji na matumizi ya Umeme kwa wananchi na utachangia kutunza mazingira kwa kuwa watu wataacha kupikia kuni na mkaa.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin