Zuena Msuya, Tabora
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amezitambulisha kampuni mbili zitakazohusika na usambazaji umeme vijijini mkoani Tabora kupitia mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, utakaotekelezwa Kipindi cha miezi 18, kuanzia Sasa.
Dkt.Kalemani amezitambulisha kampuni hizo wakati wa ziara ya kukagua baadhi ya vijiji vya mkoa huo ambavyo bado havijafikiwa na Umeme vikiwemo Miyenze na Kanyenye wilayani Uyui, pamoja na Kijiji cha Kaselya wilayani Nzega Mkoani Tabora, iliyofanyika Machi 16, 2021.
Katika ziara hiyo Dkt. Kalemani aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, pamoja na viongozi wakuu waandamizi wa Wizara.
Pamoja na mambo mengine, Dkt.Kalemani aliwataka wakandarasi hao kufanya kazi usiku na mchana kwa kasi, ubunifu na Usahihi ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa ama hata kabla ya muda huo.
Aliwasitiza wakandarasi hao kutumia vijana walio katika eneo la mradi kufanya kazi zisizohitaji taaluma maalum kama vile kuchimba mashimo, kuvuta nyaya na nyingine kama hizo ili kunufaika na uwepo wa mradi huo.
Zaidi ya shilingi Bilioni 108.2 zitatumika kutekeleza mradi wa usambazaji wa Umeme katika vijiji 299 vilivyosalia katika mkoa huo wenye jumla ya vijiji 725.
Tayari vijiji 426 vimepata umeme katika wilaya zote za mkoa huo wenye wilaya Saba.
Wilaya hizo ni Tabora Mjini, Kaliua, Uyui, Nzega, Urambo, Sikonge na Igunga.
Kampuni zilizopata dhamana ya kutekeleza mradi huo mkoani humo ni Kampuni ya kizalendo ya Sillo pamoja na Kampuni ya kigeni ya Ceylex kutoka nchini Sri-lanka.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, alitilia mkazo maelekezo yaliyotolewa kwa wakandarasi hao na kuwaeleza kuwa, Serikali imewaamini na kuwapa dhamana kubwa kutekeleza mradi huo hivyo wakamilishe kazi hiyo kama mkataba unavyoelekeza.
Wakili Byabato alisema kuwa, wakandarasi hao wakikamilisha kwa wakati mradi huo kwa kumaliza kuunganisha vijiji vyote vilivyosalia, Tanzania itaandika historia mpya kwa bara la Afrika, licha ya kuwa ya kwanza kwa kuunganisha umeme kwenye vijiji vingi kwa nchi za Afrika.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin