Salamu za rambirambi.
Bwana Yesu Asifiwe,
Tumsifu Yesu Kristo,
Moyo wangu umeugua baada ya kupata taarifa za kifo cha mpendwa wetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea Jumatano ya wiki hii, Machi 17, 2021.
Naomba nichukue fursa hii kutoa POLE zangu kwa mjane wa Rais, Mama Janeth Magufuli, wana familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote.
Kifo cha Rais Magufuli niliyemfahamu kwa miaka mingi tangu alipoingia bungeni mwaka 1995 na baadaye tukahudumu wote katika serikali ya marehemu Rais Benjamin Mkapa ni pigo kubwa kwa taifa.
Ninakumbuka namna nilivyofanya naye kazi vizuri na kwa ukaribu na kwa ushirikiano mkubwa wakati Rais Jakaya Kikwete aliponiteua kuwa Waziri Mkuu mwaka 2005.
Mwaka 2015, wote tukiwa wagombea tulishindana kwenye kinyang'anyiro cha Urais, nilimuona ni mtu mwenye maono na moyo mwema wa kutaka kuliongoza taifa hili, mtu mwenye uthubutu wa kutaka matokeo na Tanzania mpya.
Natambua na kuheshimu uchapakazi wake na namna alivyoweza kurudisha nidhamu ya watumishi wa Serikali na ujasiri wake katika ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu.
Ni wazi kifo cha Rais Magufuli kilichotokea takriban miezi minne tu tangu aingie madarakani katika muhula wake wa pili wa urais kimeliacha taifa katika simanzi kubwa kwa kumpoteza kiongozi shupavu, mzalendo wa kweli, mtetezi wa wanyonge na mchapakazi hodari asiyechoka.
Nitumie fursa kuwaomba Watanzania wenzangu kusimama pamoja na kuliombea taifa amani, umoja na mshikamano wa dhati wakati wote wa kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kumpoteza Jemedari wetu Rais Magufuli.
Si jambo rahisi kwa nchi kumpoteza kiongozi wake mkuu wakati akiwa madarakani.
Kwa sababu hiyo tunapaswa kusimama pamoja na Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kumuombea aweze kusimama imara na kuliongoza taifa kwa weledi na hatimaye kutuvusha salama.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina lake Lihimidiwe!
Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu