Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, tatizo la kukatika umeme mara kwa mara ambalo lilijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini siku za hivi karibuni limemalizika.
Akizungumza na wakazi wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo, Makamu wa Rais amesema kuwa tatizo hilo limemalizika baada ya mitambo iliyokuwa na hitilafu kufanyiwa matengenezo.
Amesema tayari amezungumza na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na amemuhakikishia kuwa umeme hautakatika tena.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alilazimika kumpigia simu Dkt Kalemani baada ya wakazi wa wilaya ya Korogwe kulalamikia tatizo la kukatika umeme mara kwa mara.
Amefafanunua kuwa tatizo hilo la kukatika kwa umeme mara kwa mara lilijitokeza kutokana na mitambo ya kufua na kusambaza umeme kupata hitilafu, na hivyo kulilazimu Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kufanya matengenezo.