Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi
**
Jeshi la Polisi mkoani Kagera linaendelea kuchunguza tukio la vifo vya watu watatu lililotokea Machi 26, 2021, saa 9:00 usiku katika kijiji cha Mayondwe wilayani Muleba.
Katika tukio hilo baba wa familia aliwaua mke wake na mtoto wake mmoja kwa kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao na kisha naye kujiua kwa kujinyonga kwa shuka.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi ametaja waliopoteza maisha kuwa ni Editha Martin (48) na Sawia Sudi (25) ambao walikatwa kwa panga na mtuhumiwa Sudi Mwamandi (49) ambaye baada ya kufanya mauaji hayo alijinyonga kwa kujitundika juu ya mti kwa kutumia shuka.
Kamanda Malimi amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa kifamilia, uliotokana na mke wa mtuhumiwa Editha Martin na mtoto wake Sawia Sudi kubadilisha dini kutoka Uisilamu na kuwa Wakristu.
"Kitendo hicho inaonekana kilimkasirisha sana baba wa familia, na mama alipoona ugomvi umezidi alihama na kwenda kuishi sehemu nyingine, na siku ya tukio mtuhumiwa huyo alivamia katika nyumba walikohamia na kumkuta mke wake ambaye alimkata kwa panga na wakati akitoa alikutana na binti yake naye akamkata kwa panga na kusababisha vifo vyao papo hapo", amesema.