Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo amesema hadi sasa nchi na mipaka yake ni salama na wataendelea kumlinda Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CDF Mabeyo ameyasema hayo leo Machi 26,2021 wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Joseph Magufuli Wilayani Chato mkoani Geita ambapo amesema kuwa kwa niaba ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini anahakikisha uimara wa ulinzi na usalama ambao pia utaendelea kuimarishwa.
"Tutaendelea kukulinda ukiwa Rais wa Tanzania na Amiri jeshi mkuu na sio Amirati kama ilivyokuwa inapendekezwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kukutii na kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania'', amesema CDF Mabeyo.
‘’Tunakuahidi utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kama ilivyo ada ya mila na desturi ya majeshi yetu katika awamu zote zilizopita kwa manufaa ya ulinzi, usalama na ujenzi wa taifa letu’’. alisema Jenerali Mabeyo.
Aidha Mabeyo amesema vyombo vya ulinzi vinamhakikishia Rais Samia uadilifu, utii na uaminifu kwa mujibu wa mila na desturi za majeshi katika kuhakikisha ulinzi na usalama kama ilivyokuwa katika awamu zote za uongozi.Kuhusu namna alivyomfahamu na kufanya naye kazi hayati Magufuli Jenerali Mabeyo alisema;
‘’Aliviamini na kuvipenda vyombo vya ulinzi na usalama alihakikisha kuwa anaviwezesha kwa mahitaji ya kiutendaji na utawala ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa.’’
‘’Alisema hatuwezi kuwa na vyombo vya ulinzi imara bila kuwa na uchumi madhubuti, hatuwezi kutegemea misaada ya kuimarisha vyombo vyetu lazima tuimarishe uchumi wetu ili tuweze kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.’’
Mabeyo amesema walishiriki katika kulinda mgodi wa Tanzanite, na kabla ya kulinda, kujenga ukuta kuzunguka mgodi huo.
Pakua / Download App ya Malunde 1 blog Tuwe tunakutumia taarifa zote moja kwa moja kwenye simu yako bure kabisa
Social Plugin