Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maji kutoka katika vyanzo vya maji vya muda mrefu katika maeneo yao Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) imependekeza kutumika kwa maji ya Ziwa Tanganyika kwa timu ya mtandao wa maji kitaifa inayoshughulikia upatikanaji wa maji kutoka katika vyanzo vya uhakika kufanya upembuzi wa mapendekezo hayo na kuanza kutekelezwa.
Akieleza mipango hiyo Mkurugenzi wa SUWASA Mhandisi Gibon Nzowa alisema kuwa mpango huo wa kutoa maji katika ziwa Tanganyika kutokea katika Kijiji cha Kasanga, Wilayani Kalambo umelenga kuhudumia wananchi wanaoishi ndani ya mita 12 katika vijiji vitakavyopitiwa na bomba la maji litakalofikisha maji katika mji wa Sumbawanga, na miji midogo ya Matai, Namanyere na Laela.
“Mapendekezo yetu ni kuchukua maji Kasanga, kwasababu tukiangalia hata gharama za uendeshaji hapo baadae yale maji yaje kwa lengo kwanza kunufaisha mji wa Sumbawanga, kwasababu vyanzo vyetu na sisi sio vya muda mrefu, na bomba hilo litakuwa linahudumia umbali wa km 12 kila upande katika vijiji vyote bomba kuu litakapopita, likiwa linakuja Sumbawanga litapita mji wa matai, litakuja Sumbawanga, litaenda Chalan a Mji wa Namanyere, nah uku litaenda Laela mpaka kwa wenzetu Tunduma,” Alieleza.
Mpango huo umewekwa bayana baada ya Wabunge wa Mkoa wa Rukwa kupendekeza kutumika kwa maji ya Ziwa Tanganyika baada ya kuonekana vyanzo vingi vinavyotegemewa na Wakala ya Usambazaji Majina Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) mkoani Rukwa kuwa ni vya mserereko na kutegemea mito ambayo shughuli za kibinadamu zimeendelea kuhatarisha uwepo wa vyanzo hivyo.
Akizungumza katika kikao hicho cha Uwasilishaji wa Hali ya upatikanaji wa huduma za maji vijijini Meneja wa RUWASA mkoani Rukwa Mhandisi Boaz Matundali alisema kuwa wanamkakati wa kuweza uzio au mabango katika vyanzo hivyo vya maji ili wananchi wasiweze kuharibu mazingira hayo.
“Lakini kwa kiwango kikubwa tunategemea kushirikiana na halmashauri zetu Pamoja na ofisi za Bonde la Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika kuhakikisha kwamba vyanzo vyetu vinatunzwa na miti yetu haikatwi hovyo ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwepo wa maji kwa muda mrefu na miradio yetu kuwa endelevu,” Alimalizia.
Aidha, katika nyakati tofauti wabunge hao nao walielezea kuwa mwarobaini wa uhakika wa upatikanaji wa maji katika miji na vijiji vya mkoa huo ni kuyatoa maji ziwa Tanganyika ambalo wilaya mbili katika wilaya tatu za mkoa huo zinapakana na ziwa hilo.
Mbunge wa Kwela Mh. Deus Sangu alisema, “Mkoa wetu una vijiji vingi, naangalia uendelevu wa vile vyanzo inawezekana vikafanya kazi kwa miaka mitano hadi kumi, lakini kutokana na mabadiliko watu wanazaliana, baadae vyanzo hivyo vikashindwa kuhimili kuhudumia vikaisha, mimi nashukuru utaratibu wa serikali kuanzisha hivi vikundi, lakini na sisi tufaidike kwa kuwa mkoa ambao vyanzo zitakapojengwa, baadae tuje na mpango mpana, tutafute chanzo kikubwa kitakachokuja kulisha vyanzo hivi,” Alisema.
Katika Kuongezea hilo mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Aida Khenan alisema, “lakini jambo la kutoa maji ziwa Tanganyika ni mwarobaini na kunakuwa na sababu kubwa moja, ule mradi wa ziwa Tannganyika unaweza kusambaza katika mikoa mitatu, Katavi, Rukwa na Songwe, kama maji yalitoka Ziwa Victoria kwenda Tabora, hizi km 64 kutoka Kirando kuja Namanyere je?”
Nae Mbunge wa Kalambo Mh. Josephat kandege aliongeza kuwa ni vyema wanamkoa wa Rukwa wakawa na lugha moja juu ya kushinikiza kuupata mradi wa maji kutokea ziwa Tanganyika ikiwa ni Pamoja na ziwa hilo kufurika na kusababisha maafa katika vijiji vilivyopo karibu na ziwa hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo mradi huo sio mgeni kwani umeshaanza katika Kijiji cha Kirando na kuhudumia vijiji vichache na kusisitiza kuwa endapo utakuwa ni mradi mkubwa maana yake ungekuwa na manufaa makubwa ndani ya mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani.
“nadhani ipo haja ya kuandika andiko kubwa la mradi halafu tushirikiane Pamoja na waheshimiwa wabunge wetu tupige debe halafu tuweze kupata hayo manufaa mapana, tutakapokuwa na uhakika wa maji hata viwanda vikubwa vikiwepo huku kwetu vinaweza visitetereke, lakini kwa hali ya sasa mtu anaweza kuleta kiwanda kikubwa huku na maji ni changamoto hii inafadhaisha hata upande wa uwekezaji,” Alisema.
Mahitaji ya maji mkoani Rukwa yakikadiriwa kufikia lita 31,532,550 kwa siku,ambapo katika maeneo ya vijijini ni lita 25,917,500 na miji midogo ikiwa ni lita 5,615,050 huku katika Manispaa ya Sumbawanga ikihitaji lita 13,000,000, hali ya upatikanaji wa huduma hiyo katika eneo linalosimamiwa na RUWASA hadi kufikifia mwezi Januari, 2021 ni 63% na eneo linalosimamiwa na SUWASA ni 80% na kufanya mkoa kuwa na 65%.