Kisura mmoja aliyeolewa miezi mitatu iliyopita katika boma moja eneo la Iriani, Tharaka nchini Kenya amejikuta matatani baada ya kupewa talaka alipokataa kufanyiwa tambiko na mganga dhidi ya mahasidi.
Penyenye zinasema kuwa dada alifanyiwa harusi ya kufana na mumewe na wakaishia mjini ila kile ambacho hakufahamu ni kuwa familia ya mumewe ilikuwa ikiamini ushirikina.
Kwa mujibu wa Taifa Leo, mwezi mmoja baada ya wawili hao kuishi katika ndoa babaake jamaa alimpigia simu akimtaka ampeleke mkewe nyumbani.
“Mnafanya makosa makubwa kuendelea kukaa mjini bila kufanyiwa tambiko kuwakinga na maovu. Fungeni safari haraka mje nyumbani, nishalipa mganga na yuko tayari kuwahudumia,” baba alimuarifu mwanae.
Duru zinaarifu kuwa jamaa alianza kumuandaa mke kwa safari ya kuelekea nyumbani lakini alijawa na wasiwasi kumueleza haswa ni nini kilichokuwa kinawapeleka huko.
Walipofika nyumbani waliwakuta jamaa wengine wa familia wakiwa wamefika tayari na siku hiyo kila mmoja alitakiwa kuingia kwenye chumba alichokuwa mganga pekee yake.
Zamu ya mwanamke ilipofika alisita kuingia katika chumba hicho akitaka kuelezewa ni kwa sababu gani haswa alitakiwa kuingia chumbani humo.
Duru zinaarifu kuwa baada ya mvutano wa dakika kadhaa, mpiga ramli alishikwa na hasira akisema alikuwa na shughuli nyingine.
Inaarifiwa kuwa dada alikataa kata kata kufanyiwa ganga ganga hizo huku mpiga ramli huyo akionya kwamba bado kulikuwepo na hatari kwa familia kwani mmoja wao alidinda kugangwa.
Wazazi wa jamaa walipandwa na mori na kumshurutisha jamaa kumpa talaka mkewe wa miezi michache na kwa kuwa alikuwa na hofu ya kutengwa na familia hakuwa na budi ila kufanya hivyo.
Semasema zinaarifu kwamba mwanamke huyo alirejea nyumbani kwa masikitiko makubwa ya kutoijua kwa ndani familia ya jamaa ambayo licha yao kufanya harusi kanisani ilikuwa inaamini ushirikina.
Jamaa alilazimika kuanza upya safari ya kumsaka kidosho mwingine.
Social Plugin