Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mkoani Shinyanga katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Na Marco Maduhu, Shinyanga.
Serikali mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, likiwamo Shirika la Investing in Children and Their Society (ICS), ambalo linajishughulisha na utekelezaji wa miradi ya utetezi wa haki za wanawake na watoto mkoani hapa, wameadhimisha siku ya wanawake duniani.
Maadhimisho hayo yamefanyika Machi 8, 2021 katika kijiji cha Kangeme Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, na kuhudhuliwa na wadau wa maendeleo kutoka mashirika mbalimbali, watumishi wa Serikali, pamoja na wananchi, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Telack amewataka wanawake mkoani Shinyanga wajitume kufanya kazi kwa bidii, pamoja na kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali, na kupata mitaji ya kuanzisha biashara mbalimbali kupitia fedha za Halmashauri asilimia 10, ili wajikwamue kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi kwa waume zao.
Amesema mwanamke ni nguzo katika familia, ambapo akitetereka familia inayumba pamoja na watoto kuishi mazingira magumu, na hivyo kuwataka waache kubweteka bali wajitume kufanya kazi bila ya kukata tamaa, huku wakishirikiana na waume zao kufanya maendeleo.
“Licha ya baba kuwa ndio kichwa cha familia, lakini mwanamke yeye ni nguzo katika familia sababu hawezi kutelekeza watoto wake kama wanavyofanya wanaume kutokana na kujua uchungu wa kuzaaa, hivyo mkiwa imara kiuchumi maisha yenu yatakuwa mazuri sana pamoja na kujawa na amani,”amesema Telack.
“Fedha zipo za mikopo bila riba kwenye Halmashauri, hivyo jiungeni kwenye vikundi vya ujasiriamali, ili mpate kukopesheka na kupata fedha za mitaji na kuanzisha biashara mbalimbali na kujikwamua kiuchumi, na kuacha kuwa tegemezi kwa waume zenu bali mjisimamie nyie wenyewe,”ameongeza Telack.
Katika hatua nyingine alikemea vitendo vya wananchi kuendekeza mila na desturi kandamizi, ambazo zimeendelea kuwa chanzo cha kuwepo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, vikiwamo vipigo kwa wanawake, kukatisha ndoto za watoto wa kike kwa kuwaozesha ndoa za utotoni, na kuonya kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua watu wa namna hiyo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, akisoma taarifa ya mkoa kwenye maadhimisho hayo ya wanawake duniani mkoani Shinyanga, ametaja takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia, kuwa kuanzia kipindi cha Julai 2019 hadi Desemba 2020 yametokea matukio 10,354.
Amefafanua kuwa matukio ya ukatili wa kingono yalikuwa 832, Kisaikolojia 4,092, kimwili 1,655, kiuchumi 366, utelekezwaji familia 3,409, na kubainisha kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto hizo za matukio ya ukatili, kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali mkoani humo ili jamii ibaki kuwa salama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Investing in Children and Their Society (ICS) la mkoani Shinyanga Kudely Sokoine, amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia, ambapo pia wanatekeleza mradi wa kumaliza matukio hayo dhidi ya wanawake na watoto.
Pia ametoa wito kwa wanawake na watoto waache uoga, bali wawe wanatoa taarifa juu ya matukio ya ukatili ambayo wanafanyiwa, ili wapate kusaidiwa kuliko kukaa kimya hadi wanapata madhara ndipo taarifa zinatolewa, huku tayari wakiwa wamesha umia.
“Shirika letu la ICS, limekuwa likifanya kazi kwa ukaribu sana na Serikali ili kuhakikisha jamii yetu inaondokana kabisa na matukio ya ukatili na kuishi salama, na hata sasa kuonyesha namna gani tupo karibu na Serikali, tumechangia Sh. 200,000 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika Zahanati ya Ulowa, na hapo awali tumeshatoa michango yetu mingi tu, lengo letu wazazi wajifunge salama,” amesema Sokoine.
Nao baadhi ya wanawake ambao walihudhuria kwenye maadhimisho hao akiwemo Ester John kutoka kijiji cha Kangeme Kata ya Ulowa- Ushetu, alipongeza Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kutokomeza matukio hayo ya ukatili wa kijinsia, na kuomba elimu izidi kutolewa zaidi hasa maeneo ya vijijini ambapo bado kuna ukatili mkubwa.
Aidha mashirika mengine ambayo yalishiriki kwenye maadhimisho hayo ni Thubutu Africa Intiative, Agape, Shidepha, Rafiki SDO, PACESH, HUHESO Foundation, Msichana Initiative, pamoja na kampuni ya vinywaji ya Jambo.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mkoani Shinyanga katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama. Picha na Marco Maduhu - Malunde 1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake.
Katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, akitoa taarifa ya mkoa kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake.
Mkurugenzi wa Shirika la Investing in Children and Their Society (ICS)Kudely Sokoine, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake.
Mkurugenzi wa Shirika la Investing in Children and Their Society (ICS)Kudely Sokoine, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake, na kuwataka wanawake na watoto watoe taarifa juu ya matukio ya ukatili, ili wahusika wachukuliwe hatua na kukomesha vitendo hivyo.
Bango la siku ya maadhimisho ya wanawake duniani katika Mkoa wa Shinyanga , yaliyofanyika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Wanawake wakiwa kwenye maadhimisho yao.
Maadhimisho siku ya wanawake yakiendelea.
Maadhimisho siku ya wanawake yakiendelea.
Maadhimisho siku ya wanawake yakiendelea.
Maadhimisho siku ya wanawake yakiendelea.
Maadhimisho siku ya wanawake yakiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, kushoto akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiburudika na akina mama kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake.
Burudani zikiendelea, ambapo mwenye kaunda suti nyeusi ni katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, na mwenye ushungi ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.
Burudani zikiendelea.
Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 blog.
Social Plugin