Wanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Bugosi kata ya Nyamisangura wakiwa darasani kama walivyokutwa na mwandishi wetu
Na Dinna Maningo,TARIME
Walimu wa shule ya msingi Bugosi kata ya Nyamisangura wilayani Tarime mkoa wa Mara wanalazimika kukaa nje kwenye korido/ kibaraza cha darasa wakisahihisha madaftari ya wanafunzi kutokana na ukosefu wa Ofisi ya walimu kwa kuwa darasa lililokuwa likitumika kama ofisi ya walimu linatumiwa na wanafunzi wa darasa la awali.
Akizungumza kama mwananchi wa mtaa wa Bugosi wakati mbunge wa jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki akisikiliza kero za wananchi wa kata ya Nyamisangura kwenye mkutano uliofanyika kwenye mtaa wa Bugosi, mmoja wa walimu wa shule ya msingi Bugosi alisema kuwa shule haina ofisi ya walimu ambapo hulazimika kukaa kwenye veranda kusahihisha madaftari.
"Mhe. mbunge sisi walimu tuna changamoto ya ukosefu wa ofisi tunalazimika kukaa kwenye veranda nje ya darasa kusahihisha madaftari, tunaomba utusaidie tuwe na ofisi ya walimu tunapata shida tunapotaka kusahihisha madaftari ya wanafunzi",alisema Mwalimu huyo.
Alisema kuwa kuwepo kwa uhaba wa vyumba vya madarasa inashusha taaluma kwa wanafunzi pamoja na uhaba wa walimu na kuomba mbunge awasaidie mchango kwa kuwa wananchi wamekuwa wakijitahidi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bugosi William Marwa alisema kuwa shule hiyo ilijengwa 2014 na mwaka 2015 ilisajiliwa rasmi ina madarasa sita na kwamba bado ina upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukaa juu ya mawe na wengine kukaa kwenye ndoo za kuchotea maji na vidumu vya maji.
"Shule ilijengwa na wana mtaa na serikali ikatuunga mkono na sasa bado tunaendelea na ujenzi tumejenga madarasa mawili na ofisi moja ambayo yapo kwenye hatua ya lenta,darasa lililokuwa linatumika kama ofisi walipewa kwa muda lile ni darasa la awali wanafunzi wakiondoka baadhi ya walimu wanaingia wanakaa wengine wanakaa nje ya darasa",alisema Marwa.
Ukosefu wa ofisi ya walimu ukamlazimu mbunge Kembaki kuahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kupitia fedha za mfuko wa jimbo ili kujenga madarasa na ofisi kuondoa adha hiyo inayowakabili walimu na wanafunzi.
Mwandishi wa habari hizi alipotaka ufafanuzi katika uongozi wa shule hiyo kuhusu changamoto mbalimbali za shule ,mratibu wa elimu kata ya Nyamisangura na mkuu wa shule ya msingi Bugosi walikataa kuzungumza kwa madai wao siyo wasemaji bali msemaji ni mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Tarime au hadi wawe na kibali cha mkurugenzi.
Mwandishi wa habari aliwasiliana kwa simu na mkurugenzi wa halmashauri ya mji Tarime Elias Ntiruhungwa kufahamu hatua za zinazochukuliwa na halmashauri kuhakikisha inatatua kero za shule ukiwemo upungufu wa madawati pamoja na kutoa kibali cha kuruhusu mwandishi wa habari kuzungumza na uongozi wa shule, alisema kuwa mapungufu ya vyumba vya madarasa na ofisi ni tatizo la nchi nzima na kutaka habari hiyo isiandikwe.
Siku moja baada ya mkutano wa mbunge Kembaki kuzungumza na wananchi kusikiliza kero zao, Mwandishi wa habari hizi alifunga safari hadi shule ya msingi Bugosi ili kuona mazingira halisi ya shule hiyo na kushuhudia baadhi ya walimu wakisahihisha madaftari wakiwa wamekaa nje ya veranda la darasa na darasa lililokuwa limeandikwa ofisi ya walimu likitumiwa na wanafunzi wa awali likiwa na vitendea kazi vya wanafunzi wa awali, baadhi ya wanafunzi wakiwa wameketi juu ya mawe na kwenye ndoo.
Pia alibaini kuwepo kwa Ofisi iliyopo ni ya mwalimu mkuu wa shule huku mpishi wa chakula akipika chakula juani ndani ya darasa ambalo halijakamalika ujenzi.
Wanafunzi wa darasa la sita wakiwa darasani
Baadhi ya walimu wakiwa nje ya veranda wakisahihisha madaftari kutokana na kutokuwepo ofisi ya walimu kwa kuwa darasa lililokuwa likitumika kama ofisi linatumiwa na wanafunzi wa darasa la awali, wanafunzi wakiondoka ndipo walimu hulitumia
Social Plugin