Charles James, Michuzi TV
JEMEDARI Ameondoka! Ndio ni huzuni, vilio na simanzi kila pembe ya Tanzania, kila pembe ya Afrika na hata Dunia nayo imezizima. Mzalendo mwenye mapenzi na Tanzania yake, Rais Dk John Magufuli amelala usingizi wa milele.
Taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan inaeleza kuwa Rais Dk Magufuli amefariki Dunia jana Machi 17 majira ya saa 12 za jioni katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipokua amelazwa tangu Machi 6 akipatiwa matibabu.
Tarehe hii 17 Machi ni mwezi mmoja tangu Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad atangazwe kufariki Dunia ambapo nae alikua amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akipatiwa matibabu ya maradhi yaliyokua yakimsumbua.
Kifo cha Maalim Seif kilitangazwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Februari 17 mwaka huu.
Aliyekua Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi nae alitangazwa kufariki siku hiyo hiyo ya Februari 17 ikiwa ni siku moja yeye na Maalim Seif.
Hivyo Tarehe 17 inabaki kuwa tarehe iliyoleta majonzi kwa watanzania na kuitikisa Dunia kwa ujumla kwani imeshuhudiwa viongozi wake wawili, Rais Dk Magufuli, Maalim Seif na Balozi Kijazi wakifariki ndani ya tarehe hiyo.
Social Plugin