Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Mhandisi. James Kilaba
***
*Kanuni zaruhusu watumiaji kuhamishiana 'uniti' za vifurushi
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) imeandaa kanuni ndogo ambazo zitawezesha kutatua kero za watumiaji wa huduma na kuongeza ustawi wa sekta ya mawasiliano ikiwemo ya mtoa huduma kuweka utaratibu au mfumo wa kumwezesha mtumiaji wa huduma kuhamisha uniti za kifurushi kwenda kwa mtumiaji mwingine ndani ya mtandao wake kwa masharti mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Mhandisi. James Kilaba amesema TCRA imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikihusisha watoa huduma ili kushusha bei ya simu za kawaida ambazo ni bei ya nje ya vifurushi, na kanuni hizo zitaanza kutumia Aprili 2, mwaka huu.
Mhandisi Kilaba amesema, Februari 5 mwaka huu TCRA ilitoa matangazo ya kukaribisha maoni ya wadau wote wakiwemo watoa huduma, watumiaji na Serikali kuhusu huduma za vifurushi vinavyouzwa na watoa huduma kwa wateja ili kuhakikisha ufanisi na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kulingana na thamani ya fedha ya malipo yaliyofanywa na wanaojiunga na vifurushi husika na jumla ya maoni 3,278 yalikusanywa.
"Moja ya kanuni ya ni mtoa huduma kuweka utaratibu au mfumo wa kumwezesha mtumiaji wa huduma kuhamisha uniti za kifurushi kwenda wa mtumiaji mwingine ndani ya mtandao wake kwa masharti kwamba.....kiasi cha chini cha kuhamisha kitakua 250 Mb na mtumiaji anaweza kuwahamishia watumiaji wasiozidi wawili na mtumiaji aliyehamishiwa kifurushi hataruhusiwa kumhamishia mtumiaji mwingine uniti hizo au sehemu ya uniti alizohamishiwa." Ameeleza Mhandisi Kilaba.
Akieleza kanuni nyingine ambazo watoa huduma watatakiwa kuzifuata Kilaba amesema mtoa huduma hatatoa huduma bila kibali maalumu cha Mamlaka hiyo.
Aidha mtoa huduma atahakikisha kwamba bei za vifurushi zinazingatia bei husika ya chini na juu zilizowekwa na Mamlaka hiyo pamoja na mtoa huduma kutumia lugha rahisi na vigezo na masharti yaliyo wazi kuhusu vifurushi vinavyotolewa.
Aidha amesema, mtoa huduma anatakiwa kutoa fursa kwa mtumiaji wa huduma za mawasiliano kuchagua na kujiunga na vifurushi visivyokuwa na ukomo wa muda wa matumizi vitakavyopatikana kwenye Menu kuu, na watoa huduma wote watatumia jina linaalofanana kwa vifurushi hivyo ili vitambulike kwa wepesi na hiyo ni pamoja na kutoondolewa, kurekebishwa au kubadilishwa kwa vifurushi ndani ya siku 90 tangu kuidhinishwa kwake.
Vilevile kanuni hizo zinawataka watoa huduma kutoa taarifa pindi matumizi ya kifurushi yatakapofikia asilimia 75 na 100 kwa vifurushi vya muda wa maongezi, data na ujumbe mfupi (Sms) Pamoja na kutopunguza kasi ya mtandao katika kifurushi na hilo ni sambamba na watoa huduma kuweka programu Rununu ili kuwawezesha watumia huduma wenye simu janja kufuatilia matumizi yao ya data kwa kupakua Programu Rununu hiyo kutoka kwa mtoa huduma.
Kanuni nyingine iliyoandaliwa na Mamlaka hiyo ni kwa watoa huduma kuweka utaratibu unaowawezesha watumiaji wanaojiunga na huduma za vifurushi kuchagua na kukubali kutozwa gharama zisizokuwa kwenye vifurushi mara muda wa vifurushi wanavyojiunga au uniti za kifurushi husika kumalizika.
"Utaratibu huu wa kuchagua na kukubali utakuwa chaguo msingi mpaka pale anayejiunga achague na kukubali kutumia gharama nje ya kifurushi pindi kifurushi husika kinachoisha muda wa matumizi" Amesisitiza Kilaba.
Pia Kilaba amesema, watoa huduma waweka utaratibu wa kumwezesha aliyejiunga na kifurushi chochote kuendelea kutumia muda au uniti za kifurushi ambazo zitakuwa zimesalia ndani ya muda wa matumizi uliowekwa kwa kununua tena kifurushi hicho hicho kabla ya kumalizika muda wake.
Kilaba ametumia wasaa huo kuwakumbusha watanzania juu ya mapambano ya utapeli mtandao kwa kutokubali kutapeliwa kwa kutekeleza maelekezo yanayohusu miamala yoyote ya kifedha katika simu zao kwa kupigiwa simu kwa wanaojifanya ni wafanyakaziwa Kampuni yoyote ya simu na kuwataka kutuma namba za wanaopiga kwenda namba 15040 bure, na kwa wanaotumiwa jumbe fupi za utapeli wasitekeleze bali watume (Forward) jumbe hizo na namba za waliowatumia kwenda namba 15040.
Pia amewahimiza Watanzania kuhakiki namba zao walizosajili kwa kitambulisho cha Taifa kwa kubonyeza *106# kisha kuchagua namba 2 na kuangalia namba zilizosajiliwa kwa vitambulisho vyao na kuchukua hatua za kuzifuta kwa alama ya vidole kwa watoa huduma endapo watakuta namba ngeni zilizosajiliwa kwa vitambulisho vyao.
CHANZO - MICHUZI BLOG
Social Plugin