WAZIRI MHAGAMA ATOA WIKI MBILI CHANGAMOTO MRADI WA MKULAZI KUTATULIWA


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameiagiza kamati elekezi ya Kusimamia Mradi wa Mkulazi Estate, kuhakikisha ndani ya wiki mbili ujenzi wa barabara na uwekaji umeme kwenye eneo la mradi huo, ili kuruhusu shughuli za utekelezaji wa mradi huo za kuzalisha tani 200, 000 za sukari kuanza kama zilivyopangwa.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo wakati alipokagua shughuli za mradi huo unaotekelezwa katika shamba Na. 217 lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini. Amefafanua kuwa kamati hiyo kushindwa kutatua changamoto za barabara na umeme kwa wakati, kunasababisha matarajio ya mradi huo ya kushindwa  kuzalishwa hapa nchini, hivyo ameitaka kamati hiyo ndani ya siku mbili ikiwa ni Jumanne ya tarehe 16 Machi, 2021 kuwasilisha mpango wa namna watakavyo tatua changamoto hizo  kwa wiki mbili.

“Maamuzi yalifanyika Novemba na hadi leo Machi hakuna kilichofanyika kwenye kufuatilia. Nataka mwezi huu wa tatu kabla haujaisha mitambo ianze ujenzi wa barabara hapa na nataka majibu ya lini shughuli za kuweka umeme hapa zinaanza. Huu ni mradi wa kimkakati kwani tunao upungufu wa tani 200,000 za sukari ambazo zitazalishwa hapa.Kama hakuna kitakacho fanyika nitachukua hatua kwenu, tumekubaliana tunaenda na mwendo wa ujenzi wa viwanda na hiki nikiwanda muhimu sana” Amesisitiza Mhagama.

Akieleza changamoto zinazosababisha utekelezaji wa Mradi huo usianze, Mwenyekiti wa bodi ya Mradi Dkt. Hildelitha Msita, amebainisha kuwa changamoto ya umeme tatizo lake kubwa lilikuwa ni kwenye makubaliano kati ya Mradi na TANESCO juu ya gharama za kujenga njia za umeme huo kwa kuwa TANESCO njia hiyo haikuwa kwenye bajeti yao. Amesema tayari wamekubaliana na TANESCO kujenga njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 3. Mradi umekubali utatoa fedha  ambazo TANESCO  itazilipa kupitia  kwenye makato ya ankala za umeme zitakazo kuwa  zikihitajika kulipwa na mradi,  badala ya kulipwa gharama hizo kwa fedha ambazo zingelipwa na wananchi wenye uhitaji wa kujengewa njia  za umeme.

Kwa upande wake Meneja mradi Abdul Mwankemwa, ameeleza kuwa kutokuwepo kwa miundombinu mizuri ya barabara ya kuelekea shamba la Mkulazi, imesababisha mitambo ya kilmo, kazi ya kusafisha mashamba na kupanda kitalu cha miwakushindwa kufanyika. Aidha amefafanua kuwa Mradi umekamilisha kufanya upembuzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 42 na matokeo ya upembuzi huo yametumika kuomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuchukua jukumu la kujenga barabara hiyo inayopitia Chalinze-Seregeta kuelekea kwenye shamba.

Akieleza shughuli ambazo tayari zimefanyika kwenye mradi huo, amesema kazi ya kusafisha eneo la  kitalu lenye ukubwa wa hekta 250, imeanza huku eneo lenye ukubwa wa hekta 80 tayarilimesafishwa. Amefafanua kuwa utafiti wa udongo umefanyika na umeonesha kati ya hekta 60,103 za shamba la Mkulazi, eneo  lenye ukubwa wa hekta 28,000 linafaa kwa kilimo cha miwa. Pia uchunguzi wa kiasi na ubora wa maji umekamilika na watajenga mabwawa makubwa kwa ajili ya umwagiliaji.

Kampuni Hodhi ya Mkulanzi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha jumla 250,000 za sukari kwa mwaka ili kupunguza nakisi ya mahitaji ya sukari nchini. Endapo Mradi wa Mkulazi  Estate, ukianza kutekelezwa unatarajia kuzalisha tani 200,000 za sukari.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post