Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AIPA SIKU TATU KAMPUNI YA DL IELEZE SABABU ZA KUTOWALIPA WAKULIMA WA CHAI


 WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameipa siku tatu kuanzia jana Jumatano, Machi 10, 2021 kampuni ya DL iwasilishe maelezo ya kwanini hajawalipa wakulima chai fedha zao tangu mwaka jana hali inayosababisha washindwe kuhudumia mashamba yao.

Ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Machi 10, 2021) wakati akihitimisha kikao na wadau wa zao la chai kilichofanyika katika ukumbi wa Johnson, mjini Njombe.

Uzalishaji wa chai kavu umeshuka kutoka tani 37,192 kwa mwaka 2018/2019 hadi tani 28,715 kwa mwaka 2019/2020 kutokana na sababu mbalimbali.

Licha ya kutoa agizo hilo, Pia Waziri Mkuu ameitaka Bodi ya Chai Tanzania ihakikishe inasimamia ipasavyo zao hilo ili wakulima  waweze kunufaika. “Bodi wajibikeni kwa kusimamia ipasavyo bei ya chai na wawezesheni wakulima waelewe mfumo unaotumika katika kuuza zao hilo.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wawakilishi wa wakulima ambao walidai kuwepo kwa tofauti ya bei ya chai. “Suala la bei lizingatiwe, mifumo inayotumika katika kuuza chai ieleweke kwa wakulima.”

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa pembejeo, Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha pembejeo zinapatikana ili kumuwezesha mkulima kufanya kazi yake kwa urahisi na ufanisi zaidi. Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo nchini.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inatengeneza utaratibu wa kukutana na wadau ili kujua kero na changamoto zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie uanzishwaji wa vyama vikuu vya ushirika wa wakulima wa chai katika maeneo yanayolima zao hilo na vihakikishe vinakuwa na viongozi wenye nia ya dhati ya kuuendeleza ushirika huo na kuongeza tija kwa wakulima.

Kadhalika Waziri Mkuu ameiagiza Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) zihakikishe zinawafikishia wakulima miche bora na viuatilifu vinavyotakiwa kwa wakati ili waweze kuiongezea ubora chai inayolimwa nchini.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la chai zianzishe vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa wakulima, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na kuongeza uzalishaji.

Akizungumza kuhusu namna ya kuwawezesha Maafisa Ugani kutekeleza majukumu yao ipasavyo, Waziri Mkuu ameziagiza halmashauri zote zihakikishe zinawapatia usafiri wa pikipiki ili waweze kuwafikia wakulima kwa urahisi.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema wizara itayafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu pamoja na maoni ya wadau ili kuhakikisha zao hilo linaboreshwa. Kuhusu changamoto ya miundombinu ya barabara ziendazo katika mashamba ya chai ameahidi kuzungumza na TARURA ili kuhakikisha zinapewa kipaumbele.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com