WAZIRI UMMY: SERIKALI HAIJAPIGA MARUFUKU ZEBAKI


Serikali imesema haijapiga marufuku uingizaji na matumizi ya kemikali aina ya zebaki na badala yake imewataka waingizaji na wasambazaji kujisajili kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Hayo yamesema  Machi 5, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizungumza na wachimbaji wadogo eneo la Nholi wilayani Bahi mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi mazingira katika migodi.

Waziri Ummy alisema kuwa asilimia 80 ya kila kilo 100 za zebaki zinazoingizwa nchini hutumika katika shughuli za uchenjuaji hivyo Serikali inawajibika kupunguza matumizi ya kemikali hiyo ifikapo mwaka 2025.

“Ndugu zangu napenda kusisitiza zebaki si haramu na si madawa ya kulevya na wala si bangi hivyo wanaoingiza au kusambaza msijfiche hamtakamatwa. Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Madini tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha tunapata teknolojia mbadala ya kuchenjua dhahabu rahisi na isiyo na madhara,” alisema.

Aidha waziri huyo alisema ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imebainisha zebaki ni moja ya madini hatari zaidi na kuwa inahatarisha afya ya binadamu kwani inaweza kusababisha magonjwa ya saratani na figo pamoja madhara kwa wanyama na mimea.

Kwa upande mwingine aliwataka wachimbaji hao kutunza mazingira yanayozunguka migodi yao kwa kutokata miti ovyo ili kutumia katika shughiuli za uchimbaji na badala yake wapate vibali vya kuitumia miti hiyo.

Pia aliwataka waache kuchimba mashimo ovyo wakati wa kutafuta maeneo yenye dhahabu na badala yake wayafukie pamoja na kuhakikisha zebaki haisambai ovyo kwani inaweza kuleta madhara.

Waziri Ummy alisema Serikali inawatambua wachimbaji wadogo kwa kuwa wananajipatia kipato kutokana na shughuli hizo na pia wanaipatia Serikali mapato.

Aliwataka wamiliki wa migodi kuwapatia vifaa vya kujikingia wafanyakazi wao ili kuepuka madhara ya zebaki na kuahidi kujengwa kwa kituo cha umahiri wa uchimbaji ili wachimbaji wa eneo hilo wajifunze.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post