Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye baraza la madiwani Kishapu kulia ni mkurugenzi halmashauri hiyo Emmanuel Johnson na kushoto ni Anderson Mandia makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson akizungumza kwenye baraza la madiwani kulia ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu na kushoto ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo William Jijimya.
Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese akizungumza kwenye baraza hilo.
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa ukumbini
Katibu wa CCM wilaya, Lucas Nyanda akizungumza kwenye kikao hicho
Na Suzy Luhende, Kishapu
Wiki kadhaa baada ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuipa hati ya mashaka Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Madiwani wa halmashauri hiyo kwa kauli moja wameazimia kumsimamisha kazi Mweka hazina wa halmashauri hiyo, Deus Ngelanizya kwa kosa la kushindwa kusimamia mapato ya mwaka wa fedhan 2020/2021 na kusababishia halmashauri hiyo kuwa ya mwisho kitaifa kwenye makusanyo ya nusu mwaka.
Pia Makosa mengine ni kudharau maagizo ya madiwani na kuisababishia halmashauri kupata hati ya mashaka kwa mwaka 2019 /2020.
Madiwani hao pia wamemtaka Afisa Mipango wa halmashauri hiyo Mang'era Mang'era kujitathmini utendaji wake wa kazi kwa sababu ana jukumu la kufuatilia mipango yote ya halmashauri hiyo.
Maazimio hayo yamefikiwa jana Aprili 21,2021 kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo baada ya baraza hilo kukaa kama kamati na kujadili juu ya wafanyakazi hao.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo William Jijimya ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mondo amesema wameamua kutoa maazimio hayo kwa sababu wameshindwa kusimamia kikamilifu mapato ya halmashauri hiyo, hali ambayo wameisababishia kupata hati ya mashaka na kuwa ya mwisho kitaifa.
"Tumekuwa tukiwaagiza wasimamie kukusanya mapato ya ndani lakini hawasimamii kikamilifu, hivyo tumeona tuwaazimie ili wasiendelee kudharau. Hili litakuwa ni fundisho na kwa watendaji wengine wa halmashauri hii kwani mapato ni roho ya halmashauri hivyo tunatakiwa kuwajibika kila mmoja ili kuhakikisha mapato yanaongezeka", alisema Jijimya.
Diwani wa kata ya Mwamalasa Bushi Mpina alisema wameamua kuwaazimia watumishi hao kwa sababu hawasimamii fedha kikamilifu, fedha zinaingia lakini hawajui zinaenda wapi hivyo wameona ukusanyaji unaofanywa sio sahihi.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo Emmanuel Johnson amesema kama inatokea changamoto ya kusababisha hati ya mashaka idara ya fedha ilitakiwa kusaidiwa, kutoa ushauri na kuwa weledi katika suala la mapato, pia unahitajika ushirikiano wa hali ya juu katika kusimamia mapato.
"Kama miongoni mwetu ameazimiwa mwenzetu kwa changamoto ya kusababisha hati ya mashaka inatakiwa tujitathimini wote, kwani tulitakiwa kuwasaidia idara ya fedha na kuzingatia weledi na taaluma zetu kwa sababu suala la mapato ni letu sote, tunatakiwa tushirikiane ili kuondokana na changamoto hii",alisema Johnson.
Naye Katibu Tawala wa wilaya ya Kishapu Shadrack Kengese amesema ni jambo la aibu kuona halmashauri hii ina kuwa ya mwisho kitaifa na kupata hati ya mashaka, hivyo watumishi wote wanatakiwa kujituma katika kusimamia mapato na kuongeza vyanzo mbadala kwa ajili ya kuongeza mapato.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Lucas Nyanda amewapongeza kwa kusimamia vizuri maendeleo ya wananchi kwa sababu sifa ya kiongozi ni kuonyesha njia, lakini katika kusomeka kwa kupata hati ya mashaka haikutakiwa kufikia hatua hiyo, ni vizuri kutengeneza mazingira mazuri ili mapato yaweze kuongezeka.
"Ni aibu kubwa kwa sisi wanakishapu kupata hati ya mashaka hatutakiwi kufikia hatua hii hivyo kwa hili mliloliazimia na watumishi wengine watajisimamia, dhamila yetu ni kuendelea kushikamana tunatakiwa kuwa na mazingira mazuri ya kuweza kuongeza kipato chetu",amesema Nyanda.