Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesitisha shughuli za usafiri wa baharini zikiwemo safari za meli na vyombo vingine vya usafiri baharini kuanzia leo Jumamosi Aprili 24, 2021 saa tatu asubuhi.
Taarifa iliyotolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dkt Khalid Salum Mohamed inaeleza kuwa Serikali ya Zanzibar imesitisha shughuli hizo kuchukua tahadhari ya kimbunga Jobo kinachotarajiwa kupiga mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara na kisiwani Zanzibar pamoja na Mafia kesho Jumapili Aprili 25, 2021.
Inaeleza kuwa katazo hilo litadumu hadi hadi pale taarifa nyingine zitakapotolewa na mamlaka husika.
Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA imesema Kimbunga JOBO kimepunguza kasi mara baada ya kuingia kwenye mazingira ya upepo kinzani hivyo kwasasa kimbunga hicho ni hafifu.
TMA imetoa taarifa hiyo leo April 24, ikielezea mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi ambacho kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia na kusema kuwa kimbunga hicho kimekuwa hafifu kinachosafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini.
TMA imesema kimbunga hicho hafifu kinatarjia kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Pwani kadri kinavyosogea nchi kavu kwa siku ya leo tarehe 24 na kesho 25 mwezi Aprili, 2021 na kusababisha mawimbi makubwa.
Pia Mamlaka hiyo imesema maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja.
Aidha wananchi wameshauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka hiyo pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.