Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKOFU CYPRIAN KIZITO AFARIKI DUNIA



Rais Museveni na Askofu Mkuu wa Kampala Cyprian Lwanga Kizito (kulia)
****
Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Kampala Cyprian Kizito Lwanga amefariki akiwa na umri wa miaka 68, Kanisa limethibitisha.

Katika taarifa iliyotolewa na Diyosisi ya Kampala ya Kanisa Katoliki, Askofu Lwanga alipatikana chumbani mwake akiwa amefariki Jumamosi asubuhi. Chanzo cha kifo chake hakijabainishwa.

Taarifa za kifo hicho cha ghafla zimewashtua Waganda wengi ambao wametumia twitter na WhatsApp kutoa rambirambi zao.

Mapema Ijumaa, aliongoza Wakristo katika ibaada ya Ijumaa njema akishirikiana na Askofu mkuu wa kanisa la Uganda Daktari Kazimba Mugalu,kupitia Baraza la Muungano wa Madhehebu ya Wakristo nchini Uganda (UJCC), ambalo alikuwa mwenyekiti wake.

Kizito Lwanga aliyetawazwa kuwa padri wa Kanisa Katolikio 1978 alionekana kama mkosoaji wa serikali ya NRM.

ALikuwa akiangazia wazi wazi dhidi ya ufisadi, ukiukaji wa haki za binadamu na marekebisho ya katiba ya nchi ili kuondoa ukomo wa muhula na urais ili kumruhusu Rais aliye madarakani, Yoweri Museveni kuongeza muda wa utawala wake.


Mwaka 2012 aliwahi kumuandikia barua Rais Museveni akimtaka astaafu ifikapo mwaka 2016.

Kifo chake kimepokelewaje?

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine aliandika katika mtandao wa Twitter: Nimepokea kwa mshtuko kifo cha ghafla cha Dkt. Cyprian Kizito Lwanga, Askofu Mkuu wa Kampala. Itakuwa vigumu kukabiliana na msiba huu.

Mwaka 2018, Askofu huyo mkuu aliilaumu utawala wa Museveni kwa kuwatumia makasisi kumchunguza alipokuwa akipinga madai kwamba anapanga kupindua serikali.

Hivi karibuni, alilaani visa vya kukamatwa na kutekwa nyara kwa wafuasi wa upinzani.

Wakati wa uchaguzi wa mwezi Januari January 2021, alipendekeza uchaguzi kuahirishwa kwa kipindi cha miaka mitatu kutokana na janga la corona na kupanda kwa taharuki za kisiasa.

Mrengo wa upinzani ulipiga pendekezo hilo.

Katika Ibaada ya jana alimpongeza aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli kwa kazi alizowafanyia Watanzania na Jumuia ya Afrika mashariki kwa muda mfupi katika utawala wake.

Pia alisifu utawala uliopo kwa kuingia madarakani wakati huo mgumu baada ya kifo cha John Pombe Magufuli na kusema liwe funzo kwa mataifa mengine.

Katika ujumbe wake wa Ijumaa kuu hapo pia aliomba serikali kuwaachia huru waliowatekwa nyara au kukamatwa bila kufikishwa mbele ya sheria.

Askofu Lwanga alizaliwa mwaka 1953 wilayani Mukono mashariki ya mji wa Kampala.

Kifo cha Lwanga kimetokea wakati Uganda inakabiliwa na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kufuatia uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali huku upinzani ukidai kuwa baadhi ya wafuasi wao wametekwa.

CHANZO- BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com