WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Suzana Steven Chaula baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Akizungumzia kuhusu Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Mhandisi Ronald Rwakatare, Waziri Mkuu amesema suala hilo atalikabidhi kwa Mamlaka ya uteuzi.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo (Jumatatu, Aprili 19, 2021) wakati alipotembelea kituo cha Kikuu cha DART-Gerezani ambapo alionesha kutoridhishwa na utendaji wa viongozi hao.
“Tangu Mtendaji Mkuu ameingia DART ana miaka mitano hakuna hata basi moja alilonunua, na anasema hana fedha kwani abiria hawasafiri si kila siku wanapigania kule Kimara na wote wanalipa unasemaje hakuna fedha ya kununulia magari”.
Waziri Mkuu amesema kuwa tangu mradi huo ulipoanza mabasi yamekuwa yakipungua kutoka 140 hadi 85. “Watendaji wapo tu wamekaa ofisini wanapigwa na AC (viyoyozi) wananchi wanaumia. Hatuna sababu ya kumbakiza mtu kama hafanyi kazi”.
Amesema wakala huo ulianzishwa na Serikali kwa ajili ya kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi lakini viongozi hao wameshindwa kusimamia vizuri na hivyo kusababisha mradi huo kutoendelea vizuri.
Waziri Mkuu amesema mapato mengi ya Serikali yamekuwa yakipotea kutokana na uendeshaji wa wakala huo. “Kwa nini ukatishaji wa tiketi haufanyiki kwa njia ya kielektroniki kwa asilimia 100? Tiketi zinauzwa kwa vifurushi.”
“Haiwezekani watu wanafanya ujanja ujanja tu wakuja na tiketi zao za mfukoni alafu wakimaliza anauza za POS (Mashine ya Kielektroniki ya Kukusanyia Mapato) na wasimamizi wapo tu Mkurugenzi wa Fedha yupo tu ameshindwa kusimamia hili na lipo mikononi mwake”.
“Kwa nini mnauza tiketi kwa vifurushi hamtumii mashine kukata tiketi. Mnaua wakala huu kwa sababu wauzaji wa tiketi wanakuja na tiketi zao na nyingine mnazileta nyinyi. Hamuwezi kusimamia mradi huu wa kimkakati”.
Pia, Waziri Mkuu ametembelea karakana ya UDA ya Kurasini, Dar es Salaam na ameshuhudia baadhi ya mabasi ya wakala huo yakiwa mabovu na alipouliza yanakabiliwa na changamoto gani Mhandisi Rwakatare alisema yanatatizo la mfumo wa gia (Gearbox).
Hata hivyo Mheshimiwa Majaliwa alibaini kuwa magari hayo yanachangamoto nyingine na siyo gearbox pekee kwa sababu baadhi yake yalikuwa yameondolewa baadhi ya vipuri, viti pamoja na matairi.
“…Unanidanganya gearbox ndiyo imeharibika wakati magari chakavu hivi yameharibika kabisa, kama gearbox ndio tatizo mbona kwenye magari mengine mmetoa hadi viti na matairi?
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Forodha Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Njaule Mdendu ahakikishe mzigo ya wateja katika bandari hiyo inatoka kwa wakati. Ametoa agizo hilo alipotembelea Kituo cha Forodha Bandari Kavu iliyopo Ubungo mkoani Dar es Salaam.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin