Na Abby Nkungu, Singida
IMEBAINIKA kuwa malaria bado ni tatizo kubwa linalosumbua watoto mkoani Singida kutokana na takwimu za idara ya afya kuonesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanaougua ugonjwa huo na kwenda kupatiwa matibabu kwenye vituo vya huduma wana umri chini ya miaka mitano.
Hayo yalibainika juzi Aprili 25 mwaka huu Tanzania ilipoungana na Nchi nyingine Wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani chini ya kauli mbiu “Ziro Malaria inaanza na mimi–Nachukua hatua kuitokomeza”
Taarifa ya idara ya afya iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Ernest Mugeta inaonesha kuwa kati ya wagonjwa 42,262 waliougua malaria kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana na kwenda kutibiwa vituo mbalimbali vya huduma, 10,469 walikuwa ni watoto ambayo ni sawa na asilimia 33.
"Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, jumla ya watu 7,272 waliugua malaria na kwenda kutibiwa kwenye vituo mbalimbali vya huduma ambapo 2,581 sawa na asilimia 35.5 walikuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano", alifafanua Dk Mugeta.
Aidha, alitaja baadhi ya sababu zinazochangia watoto kuendelea kusumbuliwa na malaria kuwa ni pamoja na kinga yao ya mwili kuwa chini; hivyo kuwa rahisi zaidi kushambuliwa na ugonjwa huo na wazazi au walezi kutotumia ipasavyo vyandarua katika kuwakinga watoto wao dhidi ya mbu.
Hata hivyo, alisema kuwa Mkoa umeweka mikakati mbalimbali ya kutokomeza ugonjwa huo wa malaria, ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu na kuangamiza mazalia ya mbu.
“Kwa mwaka 2020 tumeweza kugawa vyandarua 817,151 ngazi ya kaya kwa halmashauri za Ikungi, Iramba, Itigi, Manyoni na Mkalama na huduma ya chandarua Kliniki kwa wajawazito hudhurio la kwanza na watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja kwa kupata chanjo ya Surua/Rubella (MR 1) kwenye vituo huduma”, alieleza Dk Mugeta.
Akinamama mbalimbali walisema kuwa pamoja na juhudi hizo za Serikali, bado kuna changamoto ya elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya chandarua katika jamii pamoja na imani potofu.
“Kweli vyandarua watu wanapewa lakini ukienda vijijini utakuta vingi vimezungushiwa kwenye uzio wa kufugia kuku au bustani za mboga. Baadhi wanadai vinapunguza nguvu za kiume na wengine eti wanaona ni sawa na kujifunika sanda”, alisema mama Rose Ntandu.
Mwito wao kwa wataalamu wa afya na wadau wengine wa mapambano dhidi ya Malaria ni kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya umuhimu wa kutumia chandarua na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo wataugua malaria; hasa watoto walio chini ya miaka mitano.