Mganga kutoka Kathwana, Tharaka Nithi nchini Kenya aliyepokea kitita cha KSh 200,000 kutoka kwa jamaa flani ili amtengenezee dawa ya kumkomesha barobaro aliyezoea kuchepuka na mkewe amelazimika kuzirejesha pesa hizo baada ya dawa yake kutofanya kazi.
Duru zinaarifu kwamba mzee alikuwa amechoka na tabia ya mkewe aliyempenda sana kugawa asali nje.
Kwa mujibu wa Taifa Leo, mzee huyo hakutaka kumkabili jamaa kwa kuwa alikuwa pandikizi la mtu ambaye angempokeza kichapo cha mbwa.
Badala yake mzee aliamua kwenda kutafuta huduma za mganga ambapo alitoa donge nono la shilingi elfu mia mbili pesa taslimu.
Inasemekana mganga alistaajabu kwani katika maisha yake ya huduma kwa wateja hajawahi pata kiasi kama hicho cha pesa.
“Mwanangu usiwe na shaka. Hapa ni maskani ya fundi. Hili suala litashughulikiwa kikamilifu. Halipo hata moja moja lilishawahi kunipiga chenga. Huyu lofa wako atakula nyasi. Wewe kamata hii dawa, uipake blanketi ambalo wawili hao hujifunika pindi wawapo kwenye gemu. Nakuhakikishia nyasi atazila,” mganga alijigamba.
Mzee alirudi nyumbani akiwa mwingi wa matumaini kuwa dawa ya kutuliza mkewe aache kuruka ruka nje ya ndoa.
Inaarifiwa kwamba pindi tu mama watoto alipoondoka, mzee alichukua dawa hiyo na kuinyunyiza kwenye blanketi na akasubiri kuona matokeo.
Hata hivyo siku iliyofuata nusra mzee azirai alipowafumania mke na mchepuko wake wakibarizi sebuleni baada ya kumaliza raundi tatu za mechi.
Jamaa hakuingiwa na baridi kwani tayari alikuwa amezoea kupakua asali hata mzee wa nyumba akiwa karibu.
Mzee aliingia kwenye gari lake moja kwa moja na kufululiza hadi kwa mganga huku akiwa na hasira.
“Nipe hela zangu sasa. Zitoe hela zangu au nikutoe utumbo,” mzee alimuungurumia mganga.
Mpiga ramli ambaye alikuwa na mipango ya kujenga nyumba hakuwa na lingine ila kuzitwaa hela hizo alizokuwa amezificha chini ya godoro akamrejeshea mzee.
Social Plugin