Catherine Nyokabi enzi za uhai wake
Ukizitazama picha maridadi za mrembo mwenye miaka 25, Catherine Nyokabi ambaye ameuawa kinyama na mpenzi wake, utatambua kwamba alikuwa mja mchangamfu.
Alikuwa mwanamke mchanga ambaye ndoto zake zilikatizwa ghafla na mpenzi wake baada ya mapenzi kugeuka shubiri.
Mama huyo wa mtoto mmoja, amepatikana ameuawa ndani ya gari eneo la Witethie, Kiambu nchini Kenya na mwili wake kukatwa vipande Jumatano, Aprili 14,2021.
Mpenzi wake Evans Karani ambaye ni mwanaume mwenye familia amekiri kumuua kwa sababu alikasirika kwamba marehemu alitaka kumuacha.
Marehemu alikuwa mama wa mtoto mmoja na kulingana na swahiba wake Ann Wanja, uhusiano huo ulikuwa umeanza kuyumba na wakati wa mauti yake, wawili hao walikuwa wamekutana kutatua tofauti zao.
Wanja alisema Nyokabi alikuwa amempenda sana Karani na kujitolea vilivyo.
Makachero wa DCI wamemtia mbaroni Evans Karani mwenye umri wa miaka 38 kuhusiana na kifo cha mpenziwe.
Kulingana na ripoti ya DCI, Evans Karani anazuiliwa kuhusiana na kifo cha aliyekuwa mpenziwe Catherine Nyokabi.
Mwili wa Nyokabi ulipatikana kwenye gari lake katika barabara moja eneo la Juja ukiwa umekatakatwa na kuchomwa kwa tindi kali.
Polisi wanashuku Karani alikuwa kwenye safari ya kuenda kuutupa mwili huo kichakani wakati gari lake lilikwama kwenye matope lakini mpango wake ulitibuka wakati gari lake lilikwama na kumfanya kukimbia.
Mvua ilikuwa imenyesha na kufanya barabara ya Bob Harris Juja kuwa mbaya na hivyo gari hilo likaingia matopeni.
Tayari Karani anaripotiwa kukiri kwa maafisa wa polisi kuwa alitekeleza mauaji hayo baada ya tofauti za kimapenzi.
Familia ya Nyokabi ilikuwa inafahamu uhusiano wake na mume wa mtu kwani Karani alikuwa amewajuza mipango yake ya kumuoa kama mke wa pili.
“Nilikuwa nawafahamu kama wapenzi kama tu uhusiano mwingine, walikuwa na tofauti zao ambapo niliwasaidia kutanzua," alisema baba yake mrembo huyo Gitonga Njogu.
"Niliwajua kama wapenzi. Na kama vile mahusiano mengine ya kimapenzi walikuwa na mizozo hapa na pale. Wiki mbili zilizopita, msichana wangu aliniambia walikuwa wametofautiana.
"Aliniambia walikuwa wameachana na nikamwambia ni sawa kwani hakuna haja ya kuwa kwenye uhusiano ambapo kuna masaibu," alisema mzee huyo.
Mshukiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji Jumatatu Aprili 19,2021.
Kulingana na taarifa kutoka kwa majirani, Nyokabi aliondoka nyumbani na kusema ameenda kukutana na mpenziwe.
Nyokabi amemwacha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita huku familia yake ikiomba haki itendeke katika suala hilo.
CHANZO - TUKO NEWS
Social Plugin