Lazaro Nyalandu akitangaza kurejea CCM leo
**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu ametangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) akisema ameamua kurejea nyumbani na kwamba Wimbo wa bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini.
Nyalandu ametangaza kurejea CCM leo Ijumaa Aprili 30,2021 wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi Dodoma.
Mara baada ya kutangaza uamuzi wake huo mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano mkuu maalum wa chama hicho tawala uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma,Nyalandu ametoa shukrani zake kwa Mwenyekiti wa chama hicho kumpokea ,kumsamehe na kumruhusu kumrejesha katika chama hicho.
“Ninampongeza rais kwa uongozi wako shupavu. Nakushukuru kwa kukubali kunipokea na kunisamehe pamoja na kuniruhusu kurejea chamani. Hakuna furaha izidiyo furaha ya mtoto arejeapo nyumbani. Wimbo wa bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini, Mzee Sumaye , Lowassa na Dk Slaa ni mashahidi wa hilo”, amesema Nyalandu.
Nyalandu ambaye ni Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu ya nne alijitoa CCM Oktoba 30, 2017 na baadaye alijiunga CHADEMA ambako alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kati.
Nyalandu alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 kwa tiketi ya CHADEMA, Lazaro Samwel Nyalandu hata hivyo aliangushwa na Tundu Lissu.
Social Plugin