PADRE LIVINUS AFARIKI DUNIA



Na r. Angela Rwezaula – Vatican.

Mtawa wa Nigeria wa Shirika la "Mater Dei" aliyekuwa amepewa wakfu wa kikuhani na Askofu Libanori kwa utashi wa Papa Francisko,mara baada ya kuomba ruhusa ya kupewa daraja la ukuhani kabla ya muda wake,kutokana na afya yake kuwa mbaya,ameaga dunia siku ya Ijumaa 23 Aprili 2021.

Amekuwa Kuhani kwa siku 23 tu tangu Alhamisi Kuu, lakini atakuwa kuhani hata milele kwa sababu ndivyo ilivyo Sakramenti ya daraja ambalo linamfananisha na Kristo kuhani ambaye anajitoa mwenyewe kama sadaka. Kwa utulivu akiwa anasindikizwa na jumuiya yake, amezima kama mshumaa Padre Livinus Esomchi Nnamani, mwenye umri wa miaka 31.

 Miaka kumi iliyopita alikuwa amejiunga na Jumuiya ya Shirika la “Mater Dei” yaani “Mama wa Mungu”, katika jiji la wa Owerri, nchini Nigeria, kwa malezi ya kidini. Mara baada ya nadhiri za kwanza, aligunduliwa kuwa na tatizo la saratani ya damu, lakini haikumfanya kutoendelea na mchakato wake wa mafunzo na maandalizi ya ukuhani ambayo mnamo 2019, yalimfikisha jijini Roma. Aliendelea na mapambano makubwa dhidi ya gonjwa hili, lakini ambayo miezi kadhaa, ugonjwa huo ulilazimisha kijana huyu kulazwa katika Kituo cha kiafya cha Group Casilino.

Akiwa hapo katika kituo cha kiafya, binafsi kwa hamu yake ya kuwa kuhani alimwandikia Papa Francisko mnamo tarehe 31 Machi, Jumatano Kuu. Alifanya hivyo alipoona kwamba nguvu zake zinaanza kudhoofika na akaomba aweze kupewa daraja la ukuhani mapema. Jibu la Baba Mtakatifu lilikuwa karibu mara moja, kwa maana lilikuja masaa machache baadaya kupitia kwa mmoja wa maaskofu wasaidizi wa Roma, Askofu Daniele Libanori. Askofu huyo huyo alikutana na Baba Mtakatifu siku iliyofuata wakati wa Misa ya Krismasi, (yaani ya kubariki mafuta matakatifu) akipokea jukumu la kuendelea siku hiyo hiyo ya Alhamisi kuu Takatifu, kumweka wakfu Padre Livinus.

Ilikuwa sherehe rahisi sana hospitalini, ikiongozwa na askofu msaidizi wa Roma, ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya mapadre wa shirika lake na wafanyakazi wa matibabu ambao walimtunza kwa mapenzi mema. Alipokea kikombe na paten na mikono yake ilipakwa mafuta na Krismasi baada ya sala ya majitoleo ambayo ilimfanya awe ‘alter Christus’ aliyebadilishwa kuwa Kristo mwingine kwa maana, ya kufanana na Yesu aliye kuhani mkuu. Kuanzia siku hiyo, alitumia nguvu zake kidogo alizokuwa nayo ili kuadhimisha Misa akiwa kitandani kwake. Aliunganisha dhabihu yake na ile ya Kristo, kama vile Askofu Libanori alivyomshauri siku ya kuwekwa wakfu. Na ndivyo alivyofanya hadi Jumatano iliyopita isipokuwa jana tarehe 22 Aprili, kwa sababu ya hali yake kuwa mbaya. Akitambua juu ya kile kilichokuwa kinamtokea, Padre Livinus aliomba kuungama na kupokea kumunio.

Asubuhi ya leo Ijumaa tarehe 23 Aprili, mkuu wake mkuu wa shirika, kuhani mwingine wa Mater Dei na kijana mmoja anayefanya mang’amuzi ya wito wake wamesali rosari ya Huruma ya Mungu karibu naye hospitalini. Mara tu, baada ya saa 5:10 asubuhi, Padre Livinus ameaga dunia na ndugu zake wa Jumuiya wamemkabidhi mikononi mwa Mamama kwa sala ya “Sub tuum praesidium”. Maadhimisho maziko yanatarajiwa kufanyika Jumatatu tarehe 26 Aprili saa 5.00 katika Parokia ya Mtakatifu Giovanni Leonardi, Sekta ya Torre Maura, Roma. Na baadaye Mwili wake utasafirishwa kurudi katika ardhi yake nchini Nigeria. Raha ya Milele uumpe Ee Bwana na Mwana wa Milele umwangazie apumzike kwa amani, Amina.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post