Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 6,2021 wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wa taasisi na Idara mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam.
"Kwa sababu najua tunapokuja watu wanakuja na mabango mbio mnakwenda kuyakusanya na kuwanyuka watu kuwapelekea mnapokujua nyie ili wasiseme yao yanayowasibu , naomba kero za wananchi zikashughulikiwe, tunapokuja na kukuta bango moja mkuu wa wilaya au mkurugenzi umekwenda na tukikuta malalamiko kwamba mnawafinya wananchi wasiseme hivyo hivyo tutashughulikiana",amesema Rais Samia.
Amesema imekuwa ni kawaida viongozi wakifanya ziara mikoani na wilayani wanapokewa na mabango ya wananchi wakilalamikia kero mbalimbali na masuala wanayolalamikia si ya kitaifa huku wananchi wanaothubutu kuonesha kero zao kupitia mabango wanakamatwa wakati mabango yale mengine wala siyo mambo au masuala ya kushughulikwa katika ngazi za juu ni masuala ya kushughulikwa huko chini.
“Kwa hiyo naomba tunapokuja huko mimi na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu tukikuta mabango basi yawe mambo ya kitaifa lakini siyo mambo ya kushughulikiwa kule chini, nataka niseme bango moja aidha Mkurugenzi au Mkuu wa wilaya amekwenda na hii haina maana mkazuie watu kuandika kero zao” amesema Rais Samia.