Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WA HABARI SIMIYU WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI


Na Derick Milton, Simiyu.

Waandishi wa habari mkoa wa Simiyu, jana wamefanya ziara ya siku moja ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyokuwa na lengo la kujifunza na kuvitambua vivutio mbalimbali vya utalii vinavypatikana ndani ya hifadhi hiyo.

Ziara hiyo ambayo iliratibiwa na Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Simiyu (SMPC) na kushirikisha waandishi wa habari 20 ambao ni wanachama wa SMPC.

Akiongelea lengo la ziara hiyo Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Simiyu, Frank Kasamwa alisema Klabu hiyo iliamua kufanya ziara hiyo ili waandishi wa habari wa mkoa huo waweze kuifahamu hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo kipande cha eneo lake kinapakana na mkoa wa Simiyu.

Alisema licha ya kujifunza, waandishi wa habari kupitia ziara hiyo watatumia nafasi zao kuhakikisha wanaitangaza hifadhi hiyo ambayo inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa nchini lakini ikiwa hifadhi inayotambulika kwa kiwango kikubwa duniani.

"Tunatambua kuwa Mwandishi wa habari anao uwezo wa kuwafikia watu wengi kwa muda mchache, kwa kutumia taaluma yake, kwa msingi huo kama Klabu tuliona ni vyema wanachama wetu waje kujifunza, lakini waweze kutangaza vivutio  vilivyopo ndani ya hifadhi hii," alisema Kasamwa.

Akizungumza na waandishi wa habari hao, mara baada ya kutembelea hifadhi hiyo na kujifunza, Afisa uhifadhi Idara ya Maendeleo ya utalii wa hifadhi hiyo James Nahonyo aliwapongeza waandishi wa habari kwa uamuzi wa kutembelea hifadhi hiyo.

Nahonyo alieleza kuwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa na mafanikio makubwa kwani shughuli za uhifadhi zimeendelea kuimarishwa huku matukio ya ujangili yakipungua kwa kiwango kikubwa.

Afisa huyo alibainisha kuwa licha ya kuwepo kwa janga ambalo limeikumba Dunia la  ugonjwa wa Covid -19, bado hifadhi hiyo imeendelea kupokea watalii kutoka nje na ndani ya nchi huku tahadhali zote zikichukuliwa dhidi ya ugonjwa huo.

Nahonyo aliongeza kuwa katika kuhakikisha watanzania wengi wanatembelea hifadhi hiyo, wameanzisha mpango wa kutembelea wananchi na taasisi mbalimbali katika maeneo ambayo yanapakana na hifadhi kuwahimiza na kuwaelimisha kutembelea hifadhi hiyo.

"Tumeanzisha mpango ambao unaitwa Nyumba kwa nyumba, mpango huu unalenga wananchi na taasisi kwenye maeneo mbalimbali ambayo yanapakana na hifadhi yetu, tumeamua kuwafuata huko moja kwa moja, kwenye maeneo yao wanayoishi waje kutembelea hifadhi yetu," alisema Nahonyo.

"Mpango huu umeanza kuzaa matunda, tulianza na Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, tumekuwa tukipokea makundi ya Wanafunzi wa shule za msingi, Sekondari, vyuo, wananchi wa kawaida kuja kwa wingi kutembelea hifadhi yetu," alieleza Nahonyo.

Afisa uhifadhi huyo aliwaomba waandishi wa habari hao, kuitangaza hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuelimisha jamii hasa watanzania kupenda kuitembelea kwani bado idadi ni ndogo ya watanzania ambao wanaitembelea.

Mmoja wa waandishi hao Berensi China akizungumzia ziara hiyo ameshukuru kwa elimu ambayo amepata, huku akiomba msisitizo zaidi kuwekwa katika kuhamasisha jamii kupenda kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com