Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TIC YASAJILI MIRADI 151 KWA MTAJI WA DOLA MILIONI 987.04 KIPINDI CHA MWEZI JULAI 2020-MACHI 2021

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za kituo hicho Jijini Dar es Salaam.    Baadhi ya watumishi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakifuatilia mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za kituo hicho leo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi akipata picha ya pamoja na waandishi wa habari katika ofisi za kituo hicho leo Jijini Dar es Salaam.

PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO

*******************************

NA EMMANUEL MBATILO

Katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Machi 2021, Jumla ya miradi 151 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambayo inatarajiwa kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 987.04 na kutoa ajira 13,857.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kituo hicho Jijini Dar es Salaam.

Dkt.Kazi amesema ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana ambapo kituo kilisajili miradi 169, idadi ya miradi imepungua kutokana na athari za janga la ugonjwa wa Corona Duniani.

"Sekta ya viwanda imeendelea kuongoza katika miradi iliyosajiliwa katika kituo cha Uwekezaji Tanzania ambapo imesajili jumla ya miradi 94 (62.25%) yenye mtaji wa jumla ya Dola za Marekani milioni 463.17 (46.9%), na inakadiriwa kutoa ajira kwa watanzania wapatao 9,220". Amesema Dkt.Kazi.

Aidha Dkt.Kazi amesema Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2021 kituo cha Uwekezaji kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi mipya 51 ambapo mtaji unaotarajiwa kuwekezwa wa Dola za Marekani milioni 451 umeongezeka kwa asilimia 63 na ajira mpya 4,272 zinazotarajiwa kuzalishwa zimeongezeka kwa asilimia 3.5 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana ambapo kituo kilisajili miradi 54.

Pamoja na hayo Dkt.Kazi amesema katika siku za hivi karibuni wawekezaji wengi na mabalozi na wawekilishi wa mashirika ya kimataifa wameonyesha kufurahishwa na mwenendo wa serikali katika suala zima la kuboresha mazingira ya uwekezaji na tayari wameanza kuonyesha nia ya kusaidia programu mbalombali za maboresho ya mazingira ya uwekezaji nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com